WAGANGA WA KUTIBU KWA NGONO WATINGWA KWA MWANASHERIA

Jalada la kesi ya waganga wa jadi wawili wanaotuhumiwa kubaka baada ya kutoa tiba kwa wanawake ili wapate watoto, kwa masharti ya kushiriki nao ngono bila kinga, limepelekwa kwa Mwanasheria wa Kanda wa Serikali kwa hatua zaidi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Englibert Kiondo aliliambia gazeti hili jana kuwa jalada hilo limefikishwa kwa mwanasheria kwa ajili ya kusomwa na kuangalia kama ataridhika na ushahidi kwa ajili ya kupelekwa kesi mahakamani.
“Jalada limekwisha pelekwa kwa Mwanasheria wa Serikali wa Kanda kusubiri hati ya mashtaka kama ataridhika na ushahidi katika kesi hiyo, kwa hiyo tunasubiri,” alisema Kamanda Kiondo.
Watuhumiwa hao ambao wako nje kwa dhamana ni Juma Hemedi (32), mkazi wa Tandika Azimio, Abrahman Mulsin (22), mkazi wa Tandika ambao vifaa vyao vya uganga vilichomwa moto mbele ya waandishi wa habari juzi.
Wanadaiwa wakishawaingilia wanawake hao kama njia ya kuwawekea dawa ya kupata watoto, wanaacha nguo zao za ndani  ziendelee kufanyiwa uganga.
Kwa mujibu wa Kamanda Kiondo,  sheria inasema mganga anapofanya tendo la ngono kama uganga, anakuwa amebaka, na hiyo ni kwa mujibu wa sheria ya kanuni ya adhabu 130 sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Kamanda Kiondo alisema pia kuwa Jalada ambalo limepelekwa kwa mwanasheria ni pamoja na la kesi ya wizi ya Maalim Kimti  Rita ambaye anajulikana pia kama Joseph Rita mkazi wa Tandika Devis Corner ambaye alimuibia mfanyabiashara milioni 11 akimwambia atafanyiwa uganga ili aweze kufanikiwa katika biashara yake.
Waganga hao wamekutwa na vipeperushi wakijidai mbali na tiba ya kupata mtoto kutibu magonjwa mbalimbali ikiwemo sukari, vidonda vya tumbo, nguvu za kiume, kukuza maumbile, kupata kazi, kufaulu mtihani, mvuto wa biashara, kumilikishwa jini na kupewa pete ya bahati.
Baada ya kupekuliwa walikutwa na nguo za ndani 22 ikimaanisha wanawake hao wameingiliwa kimwili bila kinga, vitu vingine walivyowakuta navyo ni pembe, tunguli, makopo ya dawa na vibuyu.

No comments: