HIZI NDIZO SABABU YA KUTEKETEA MOTO SOKO LA MCHIKICHINI

Miundombinu mibovu katika Soko la Mchikichini, jijini Dar es Salaaam,  lililoteketea juzi kwa moto, inadaiwa  kusababisha magari ya Zimamoto na Uokoaji kushindwa kupenya hadi katikati ulikoanzia.
Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,  Suleiman Kova, alisema taarifa za awali za polisi, zimeonesha moto huo ambao chanzo chake hakijafahamika,  ulianza katikati ya soko hilo kabla ya kuenea kwa kasi. Alisema chanzo cha moto huo bado hakijafahamika.
Alisema katika janga hilo la juzi saa 5, ambalo uchunguzi wa kimaabara unafanyika kubaini chanzo,  magari ya Zimamoto na Uokoaji ya taasisi  tofauti, yakiwemo ya Halmashauri ya Jiji, Bandari na kampuni binafsi, yalifika eneo hilo lakini walishindwa kufika katikati kutokana na miundombinu hafifu.
"Licha ya juhudi kubwa zilizofanywa na Kikosi cha Zimamoto na Shirika la Umeme Tanesco bado moto huo ulikuwa mkubwa  sana kiasi cha kuteketeza sehemu kubwa ya soko," alisema Kova na kwamba ulizimwa saa 9.
Moto huo uliteketeza bidhaa mbalimbali za wafanyabiashara wa soko hilo vikiwemo, viatu, mabegi na vifaa vya plastiki . “Baada ya kuona ni ngumu kudhibiti moto huo, walijitahidi kuhakikisha wanadhibiti moto huo usisambae kwa nyumba za raia zilizo pembezoni," alisema Kamanda Kova.
Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Soko hilo, Jumanne Kongogo  alisema asilimia 80 ya soko imeteketea. Aliomba Serikali iruhusu waendelee kufanya biashara katika eneo hilo.
Alisema thamani ya bidhaa zilizoteketea kwa moto huo hazijafahamika. Alisema wafanyabiashara wengi hawana bima ya biashara hizo jambo ambalo limewafanya wabaki njiapanda.
Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala,  Jerry Silaa, alisema wanaunga mkono wafanyabiashara kuendelea kutumia soko hilo.
''Katika soko hili wafanyabiashara wengi wakimaliza kufanya biashara, wanaacha biashara zao sokoni hapa, kwani wapo zaidi ya wafanyabiashara 2,700 waliosajiliwa na kila mtu ana watu wake zaidi ya wanane, hali hiyo imekosesha ajira kwa watu wengi,'' alisema Slaa.
Ofisa Masoko wa Manispaa ya Ilala, Athuman Mbelwa alisema soko hilo linachangia zaidi ya Sh milioni sita kila mwezi na kutoa ajira kwa watu wasiopungua 15,000.
Mfanyabiashara wa soko hilo, Jumanne Rashid alisema moto huo umemsababishia hasara  zaidi ya Sh milioni 15 alizokuwa akizitegemea kulipa Sh milioni nane ya mkopo aliochukua na kulipa ada ya shule kwa  watoto wawili.

No comments: