WAZIRI ASHAURI POMBE ZA 'VIROBA' ZIPIGWE MARUFUKU



Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Janeth Mbene amesema ipo haja ya pombe zinazouzwa zikiwa zimefungwa kwenye mifuko midogo ya plastiki maarufu kama viroba kuondolewa kwani ni janga la taifa linalosababisa ulevi kila eneo.
Waziri huyo aliongeza kuwa  pombe hizo zinauzwa kiholela  hadi katika mageti ya shule, vibanda vya simu, barabarani, maduka ya bidhaa za vyakula  na hata kwa akina mama ntilie.
Alisema pombe hiyo imekuwa ikiuzwa bila usimamizi, jambo ambalo linatishia Taifa kuwa la walevi na kuzitaka Manispaa kuangalia suala hilo kwani  limekuwa tatizo kubwa.
Naibu waziri huyo alisema kutokana na pombe hiyo kutowaletea tija watumiaji, pamoja na kuwa na athari za mazingira  ifikie mahali mapendekezo yatolewe ili viondolewe katika soko na kuwa katika mfumo wa chupa badala ya makaratasi.
Alisema mbali na pombe hizo ambazo zipo zinazozalishwa nchini, lakini zipo ambazo huingizwa kutoka nje ya nchi ambazo zinadaiwa kusababisha athari kwa watumiaji kupata majipu katika fizi.
"Ebu angalieni hili suala jamani, hivi viroba vimetapakaa kila mahali hata katika maduka yanayouza chakula ni kwanini yanaruhusiwa kuuuza bidhaa hiyo," alisema Naibu Waziri.
Alisema mbali na viroba hivyo kusababisha madhara ya kiafya lakini pia zinachafua mazingira kwani makaratasi yanayohifadhia hutupwa na kuzagaa ovyo mitaani.
Akizungumza, Mwakilishi kutoka Manispaa, Jumanne Ndaigeze alisema ni vyema tatizo hilo likajadiliwa na mapendekezo kutolewa ili pombe hiyo iondolewe na kuwekwa kwenye chupa ili kuondokana na makaratasi.
"Kwa kweli kama hali kama ndivyo ilivyo basi ifikie mahali kweli yawepo majadiliano ili pombe hiyo iweze kuondolewa," alisema Ndaigeze.

No comments: