WAVULANA WAACHA SHULE KUHUDUMIA NDOA ZAO SUMBAWANGA



Hali si shwari katika sekta ya elimu katika wilaya za Kalambo na Sumbawanga  mkoani Rukwa, baada ya kuelezwa idadi kubwa ya wanafunzi wa kiume katika shule za sekondari hukatisha masomo ili kujikita katika kutunza familia, kwani wengi wao ni waume za watu, wengine wakiwa na wake hadi watatu.
Kwa kiasi kikubwa, dhana iliyopo ni kwamba wanawake ndio wanaokatishwa masomo kutokana na sababu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kupata ujauzito au kulazimishwa kuolewa katika umri mdogo.
Hayo yalibainika  katika  kikao  cha  siku moja cha Wadau wa Elimu kilichowakutanisha Waratibu Elimu Kata, Maofisa Elimu  wa Wilaya  za Kalambo  na Sumbawanga na kufanyika juzi mjini hapa nchini ya uratibu wa Asasi isiyo ya Kiserikali  ya TMEP  kupitia  mradi  wake  wa  afya ya uzazi  na ujinsia unaotekelezwa  mkoani Rukwa  na  taasisi  isiyo ya Kiserikali ya Resource Oriented  Development Initiative (RODI).
Mkuu  wa Shule  ya  Sekondari Kasanga iliyopo katika mwambao  mwa Ziwa Tanganyika  wilayani Kalambo, Christopher Sinyangwe  ndiye aliyeibua hoja, baada ya kueleza kuwa utoro sugu  ni changamoto kubwa  katika  shule  hiyo, akisema kati ya wanafunzi 80 wanaoanza kidato cha kwanza, mara nyingi wanaohitimu hawazidi 30.
Aliongeza kuwa  sababu  kubwa  ni mwamko  mdogo  wa elimu  kwa upande  wa wazazi  na  walezi  ambao  wanawaozesha  watoto  wao  mara  tu  wanapoingia Kidato  cha Kwanza  na kuwaacha wake  zao  katika  vijiji  wanavyotoka hivyo  wanalazimika  mara kwa mara  kukatiza masomo  yao   ili  waweze kurudi  nyumbani  kuwajibika  kwa  familia  zao.
"Zipo  taarifa  za uhakika  kuwa  wanafunzi  wa kiume   kuwa na wake  wawili hadi  watatuÉbaadhi yao  wanaanza  Kidato cha Kwanza  tayari  wameshaoa, wakifika  Kidato cha Tatu  tayari  ana wake  watatu au  wawili na  watoto ambao  anawajibika  kuwahudumia  hivyo  wanakatiza masomo  na kujihusisha na  shughuli za  uvuvi  kwa muda  ili kuzikimu  familia  zao  kisha  hurejea shuleni,"  aliongeza Sinyangwe.
Kwa mujibu  wa Kaimu Ofisa Elimu  wa Halmashauri  ya Wilaya ya Kalambo, Japhet Buchwa  ambaye  pia ni Ofisa Elimu Taaluma (Sekondari) alibainisha kuwa  utoro  sugu  ni  changamoto  kubwa  shuleni  kwa  upande  shule  za  umma   watoto  600 walikatiza  masomo  yao kwa  kipindi  cha  Januari  hadi Februari  mwaka  huu.
Alisema katika kipindi  hicho cha kati ya Januari  na Februari mwaka  huu  wanafunzi  wapatao 23  kutoka  shule za sekondari  za binafsi wamekatiza  masomo  yao  kwa sababu  mbalimbali  zikiwemo  za ujauzito.
Kwa mujibu wa Buchwa, watoto  wapatao 4,913 wanasoma  katika  shule  za sekondari za  umma  wilayani humo  ambapo  shule  za sekondari  za  binafsi  zina wanafunzi  wapatao 300.
Akichangia  uzoefu  wake, Mratibu  Elimu Kata ya Mfinga  katika Bonde la Ziwa Rukwa  wilayani Sumbawanga  alibainisha kuwa   kutokana na  mwamko duni wa  elimu  wazazi  huwaozesha  watoto  wao wa kike kwa mahari  kati  ya ng'ombe  25  hadi 30  pia  kwa  watoto  wa kiume  wanarubuniwa na  wazazi wao  kukatiza masomo  yao   na kuwaajiriwa   kama  vibarua  mashambani  na kuchunga  mifugo.
"Wengi  wa wazazi  na walezi  ambao  hawaoni  umuhimu  wa  elimu  wanadai ni  bora  watoto  wao  wakaoe  au kuolewa  kuliko  kuendelea  na masomo isitoshe  baadhi  ya  wazazi  huwatishia maisha walimu wanapofuatilia watoro  sugu," alibainisha.
Naye Mratibu Elimu Kata  ya Mpui  wilayani Sumbawanga, Tabia Mkembo alibainisha  kuwa  kutokana  na  Shule ya Sekondari Mpui  kutokuwa na  uzio, wanafunzi  wa kike  wanadaiwa  kutoroka  usiku  na kwenda kufanya ufuska hivyo  baadhi yao  kupata ujauzito  maarufu kama 'mimba za minadani'.
Alidai vibarua  wa kampuni  ya  ujenzi  inayojenga  barabara  ya Laela -Ð Sumbawanga  kwa kiwango  cha  lami  ni miongoni mwa watuhumiwa wa 'kuoa'  watoto  wa kike  shuleni hapo  ambapo baadhi  ya wasichana  wanaoishi  katika hosteli  shuleni hapo  wanashawishika  kutoroka  usiku  na  kwenda  kwa 'waume' zao  hao kutokana  na  shule  hiyo kutokuwa na  uzio.
"Tuna  taarifa kuwepo  kwa visa  kwa  wasichana  wanaoishi  katika mabweni  shuleni
hapo  kutoroka  na kwenda kulala  katika  bweni  la  wavulana Hapa  walezi  wa watoto  hawa 'patroni '  na  'matroni'  wanapaswa kuwafuatilia  kwa  karibu  watoto  hawa," alisisitiza.
Kwa upande  wake Mkurugenzi  wa RODI, Gideon Mpina  alizitaka   Halmashauri kuunda  sheria  ndogo  ndogo  zitakazo zipa  nguvu  za kisheria  mamlaka husika  kuwasaka wazazi  na  walezi  wote  watakaobainika   kuwaozesha watoto  wao  wanaosoma  ili  sheria  iweze  kuchukua  mkondo  wake

No comments: