WALIOMSHITAKI PINDA MAHAKAMANI WASHINDWA KESI



Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imetupilia mbali kesi ya kikatiba iliyokuwa inamkabili Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kwa kuwa waliofungua kesi hiyo hawana haki kisheria.
Kesi hiyo namba 24 ya mwaka jana ilifunguliwa na Kituo cha Msaada wa Kisheria na Haki za Binadamu (LHRC) kwa kushirikiana na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) dhidi ya Waziri Mkuu Pinda na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Katika madai yao LHRC na TLS walidai, Pinda alivunja Katiba kutokana na kauli aliyoitoa bungeni Juni 20, 2013, wakidai ni amri kwa vyombo vya utekelezaji wa sheria ya kuwapiga wananchi wakati wa vurugu.
Akisoma uamuzi wa pingamizi la awali lililowasilishwa na Pinda na AG, Jaji Kiongozi Fakhi Jundu, alisema waliofungua kesi hiyo hawana haki kisheria kwa sababu madhara ambayo yangetokana na kauli hiyo yangekuwa kwa wananchi na siyo mashirika.
Alisema walalamikaji wangeweza kufungua kesi endapo kauli hiyo ingekuwa inaathiri mashirika, lakini kauli iliyotolewa inaweza kumuathiri mtu mmoja pia wamefungua kesi kwa niaba  ya watu wengine wakati kilichotakiwa ni mtu aliyeathirika na kauli husika ndiye awasilishe ombi au kufungua kesi.
Katika pingamizi lao pamoja na hoja nyingine, walidai kesi hiyo imefunguliwa isivyo halali kwa kuwa inakiuka Katiba na Sheria ya Mamlaka, Kinga na Haki za Wabunge, ya mwaka 1988 kwa kuwa Waziri Mkuu analindwa na Katiba Ibara ya 100 (1) na (2).
Jaji Jundu alisema kwa upande wa haki na upendeleo wa wabunge mahakama haina mamlaka ya kuhoji jambo lolote, lakini kuhusu kinga mahakama ina uwezo wa kusikiliza kwa kuwa kinga yao ina mipaka hivyo mbunge anaweza kukamatwa na kushitakiwa kwa kufuata taratibu za kisheria.
Aliongeza  kwa mujibu wa kanuni ya 71 (1)C  ya Bunge, bila kuathiri ibara ya 100, mtu yeyote ambaye ataona ameathirika na hoja au kauli iliyotolewa bungeni na mbunge anaweza kupeleka malalamiko yake kwa Spika wa Bunge na mtu huyo awe raia wa Tanzania.
Katika uamuzi huo ulioandikwa na majaji watatu, Jaji Jundu alisema kwa mujibu wa ibara ya 100 (1) wabunge wana uhuru wa kujadili jambo lolote bila kuhojiwa, lakini ibara ya 100(2) kinga ya wabunge ina mipaka na mtu binafsi anaweza kuhoji endapo kauli iliyotolewa inaweza kumuathiri.
Akizungumza nje ya Mahakama, Wakili Harold Sungusia alisema wiki ijayo jopo la mawakili waliofungua kesi hiyo litakutana na kujadili hatua watakazochukua.

No comments: