Wafanyabiashara
wawili wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
wakikabiliwa na mashitaka ya kusafirisha na kuuza meno ya tembo yenye thamani
ya Sh bilioni 5.4.
Washitakiwa
hao Salivius Matembo (39) na Manase Philemon (39) walifikishwa mahakamani hapo
jana na kusomewa mashitaka na Wakili wa Serikali, Pius Hilla akisaidiwa na
Mwendesha Mashitaka Jackson Chidunda mbele ya Hakimu Mkazi Frank Moshi.
Wakili
Hilla alidai kuwa, kati ya Januari 2000 na Mei 22 mwaka huu Dar es Salaam,
washitakiwa hao walisafirisha na kuuza nyara za serikali ambazo ni vipande 706
vya meno ya tembo vyenye gramu 1889 na thamani ya Sh bilioni 5.4 bila kuwa na
kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Aliendelea
kudai kuwa, siku isiyofahamika washitakiwa hao walikula njama za kutenda kosa
kwa kukusanya, kusafirisha na kuuza meno hayo jambo ambalo ni kinyume cha
sheria.
Katika
mashitaka mengine, Hilla alidai Mei 21 mwaka huu katika Hospitali ya Sinza
Palestina, Philemon alitoroka akiwa chini ya ulinzi halali wa askari D/koplo
Beatus.
Hakimu
Moshi alisema washitakiwa hawataruhusiwa kujibu mashitaka yao kwa kuwa mahakama
hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo na hawajapata kibali cha
kuisikiliza.
Wakili
Hilla alidai upelelezi unaendelea na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa kwa
kwesi hiyo.
Hata
hivyo upande wa utetezi ulidai kuwa hati hiyo haipo mahakamani kisheria kwa
kuwa haijasajiliwa na kuomba washitakiwa wapewe dhamana kwa sababu mashitaka
yao yanadhamana kisheria.
Akijibu
hoja Wakili Hilla alidai hayo ni mambo ya kiutawala lakini kesi hiyo imesajiliwa
kama ya Uhujumu Uchumi namba 21/2014 na kuhusu dhamana alidai kwa mujibu wa
Sheria za uhujumu Uchumi, mahakama hiyo hairuhusiwa kutoa dhamana kama
mashitaka yamehusisha zaidi ya Sh milioni 10.
Hakimu
Moshi alisema hayo yalikuwa mambo ya kiutawala lakini kesi hiyo imesajiliwa na
sheria ipo wazi kuwa washitakiwa wanatakiwa kupewa dhamana Mahakama Kuu ambayo
ndiyo yenye mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo. Kesi itatajwa tena Juni 17 mwaka
huu.
No comments:
Post a Comment