Kampuni ya ndege ya
Fastjet imetangaza kuongeza safari zake hapa nchini ambapo sasa itaruka kwenda
Mbeya mara mbili kwa siku na Mwanza mara tatu.
Meneja
wa Uchumi na Biashara wa kampuni hiyo, Jean Uku aliwaambia waandishi wa habari
jana kuwa wamefikia uamuzi huo baada ya kupokea maoni na maombi kutoka kwa
wateja wake mbalimbali nchini.
“Kwa
niaba ya shirika la ndege la Fastjet natangaza rasmi kuwa kuanzia leo huduma
zitaongezeka katika maeneo mbalimbali hapa nchini, na namna hali itakavyoruhusu
tutakuwa tukiongeza huduma hizi katika eneo la ndani ya nchi na nchi za
jirani,” alisema Uku.
Aidha
Uku aliongeza kuwa, Juni 30 mwaka huu, Fastjet itaongeza huduma zake katika
Uwanja wa Ndege ya Kilimanjaro (KIA) kwa kufanya safari kila Alhamisi na
Jumamosi mara tatu kwa siku na mara mbili kwa wiki.
Alisema
sasa wasafiri kutoka na kwenda mikoa ya Mbeya, Mwanza na Kilimanjaro
watafurahia huduma hiyo inayotokana na kuongezwa safari za ndege kwenda huko
mara mbili.
“Kuongezwa
kwa huduma hii katika mikoa iliyotajwa itaweza kuwahudumia hata wasafiri wa
nchi jirani kama vile Zambia na Malawi wanaotumia viwanja vya ndege vya
Tanzania kuingiza na kutoa bidhaa,” alisema Uku.
Kwa
upande wao wafanyabiashara wanaotumia huduma ya safari za anga wamesema kuongezwa
na kuimarishwa kwa huduma hiyo kutawasaidia kufanyikisha shughuli zao za
kibiashara kwa wakati na nafuu.
Tiketi za Fastjet zimeanza kuuzwa katika vituo mbalimbali na kupitiwa
katika mitandao ya internet ambapo tiketi ya moja kwa moja ni shilingi 32,000 bila ushuru na gharama
zinginezo kama mzigo.
No comments:
Post a Comment