WATAKA MAPATO YA GESI YATUMIKE KWENYE AFYA NA ELIMU



Asilimia kubwa ya watanzania waliohojiwa na taasisi ya utafiti wamesema mapato yatakayopatikana kutokana na gesi yatumike katika huduma za afya na elimu.
Hayo yalisemwa jana, Dar es Salaam na Mtafiti wa Taasisi ya Twaweza, Elvis Mushi wakati akiwasilisha utafiti walioufanya wakishirikiana na Benki ya Dunia.
Alisema Watanzania asilimia 43 wangependa mapato yote yaende serikalini kwa ajili ya kugharamia huduma muhimu zikiwemo za afya na elimu. Alisema wananchi wanne kati ya 10 waliohojiwa katika utafiti huo walipendekeza yatumike katika miundombinu na kupambana na umasikini.
Mushi alisema zaidi ya nusu ya Watanzania ikiwa ni sawa na asilimia 55 wangependa baadhi ya mapato ya mafuta na gesi wapewe wananchi moja kwa moja kwa fedha taslimu.
“Ili kuleta maendeleo kuna asilimia 17 ya wananchi wangependelea serikali ipate asilimia kubwa zaidi ya mapato kwa ajili ya kuendeleza miundombinu na huduma za kijamii na wananchi wagawiwe kiasi kinachobaki,” alisema Mushi.
Alisema ingawa makadirio ya sasa yanaonesha uchimbaji mkubwa wa mafuta na gesi huleta faida katika kipindi cha miaka saba hadi kumi ijayo, wananchi asilimia 36 wanaamini kuwa makampuni ya gesi tayari yanapata fedha kutokana na ugunduzi huo.

No comments: