"MRADI WA DART KUTOA FURSA YA UBUNIFU AFRIKA"



Waziri Mkuu, Mizengo Pinda  amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi za kwanza katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kuingia kwenye ubia na sekta binafsi katika mradi mkubwa wa usafirishaji abiria.
Alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam wakati akifungua
Mkutano wa Majadiliano wenye lengo la kutangaza Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka(DART) unaomalizika leo.
Waziri Mkuu alisema kutekelezwa kwa mradi huo kutatoa fursa za ubunifu utakaowezesha kupatikana kwa suluhisho la usafiri mijini na hasa kwenye miji inayokua kwa kasi Afrika.
"Mbali ya kutoa huduma za hali ya juu, za haraka na ambazo siyo ghali kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, nia ya Serikali ni kuona mfumo mpya wa matumizi ya kadi kwenye mpango huu wa usafiri unatumika ipasavyo," alisema.
Alisema ni matumaini ya Serikali kwamba wadau kutoka sekta binafsi ambao ni wazawa na wa kutoka nje ya nchi watashiriki kwenye mradi huu ili uweze kuboresha matumizi ya kadi ambayo mtu hatatakiwa kulipia fedha taslimu akiwa ndani ya basi bali kutumia kadi anayoilipia kabla ya kuingia ndani ya basi husika.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufungua mkutano huo, Waziri Mkuu alisema Serikali iliamua kuanzisha mradi huo kupunguza msongamano wa magari kwenye barabara za Jiji la Dar es Salaam.
"Hii ni awamu ya kwanza ambayo inakaribia kukamilika na inaanzia Kimara hadi Kivukoni na itakuwa na matawi mawili ya Morocco na Kariakoo. Mradi wote una awamu sita za ujenzi kuelekea maeneo tofauti ya jiji," alisema.
Mbali na mradi huo wa mabasi yaendayo haraka, Serikali inaangalia uwezekano wa kutumia usafiri wa majini kwa kutumia boti kati ya Dar es Salaam na Bagamoyo kama njia mojawapo ya kupunguza msongamano wa magari jijini Dar es Salaam.
“Vilevile tutaimarisha usafiri wa reli kama njia nyingine ya kupunguza tatizo hili. Dk Mwakyembe (Waziri wa Uchukuzi) ameanza na sote tumeona ni jambo linalowezekana. Cha msingi ni kuimarisha tu usafiri huu,” aliongeza Waziri Mkuu.
Awali, akiwakaribisha wajumbe wa mkutano huo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI),  Hawa Ghasia alisema Serikali imedhamiria kuhakikisha kuwa mradi huo unafanikiwa.
Pia alitumia fursa hiyo kushukuru Benki ya Dunia ambayo alisema imetoa kiasi cha dola za Marekani milioni 200 kwa ajili ya kufadhili mradi huo.
Mkutano huo unashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo wa ndani na wa nje wanaotarajiwa kutoa huduma za mabasi makubwa na madogo, utoaji tiketi, ulinzi, usafi na huduma za maduka.

No comments: