VIONGOZI, WAFANYABIASHARA WA DRC WATINGA NCHINI



Viongozi pamoja na wafanyabiashara kutoka jimbo la Katanga katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wamewasili nchini kwa ziara inayolenga kuimarisha uhusiano wa kibiashara kati ya nchi hiyo na Tanzania.
Ujumbe huo wa watu 16 unaongozwa na Naibu Gavana wa jimbo hilo, Yav Guilbert na Waziri wa Uchukuzi wa jimbo hilo, Kahozi Sumba.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kupokea ujumbe huo jijini Dar es Salaam juzi, Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe alisema, “Tunataka kumaliza mazungumzo tuliyoaanza ili kuimarisha uhusiano wetu”.
Mwanzoni mwa mwezi uliopita, Tanzania ilifungua ofisi ndogo ya mawasiliano ya Mamlaka ya Bandari (TPA) mjini Lubumbashi nchini DRC katika jimbo hilo la Katanga.
Ofisi hiyo inalenga kurahisisha na kuleta ufanisi katika kusafirisha mizigo ya wafanyabiashara wa DRC wanaotumia bandari ya Dar es Salaam.
Inalenga pia kusaidia wafanyabiashara wa nchi hiyo kumaliza matatizo yao Lubumbashi badala ya kusafiri hadi Dar es Salaam.
 Mienendo ya taarifa za mizigo itafanyika mjini humo na hivyo kuharakisha taratibu za mizigo bandarini Dar es Salaam.
Waziri Mwakyembe alisafiri kwa barabara kutoka Dar es Salaam hadi Lubumbashi kupitia Zambia kwa zaidi ya kilometa 2000 kuangalia na kupata taarifa za changamoto wanazokumbana nazo wafanyabiashara wa DRC kuanzia bandarini Dar es Salaam.
Kwa upande wake, Gavana Guilbert, alishukuru serikali ya Tanzania kwa mapokezi mazuri waliyopata. “Tunashukuru sana kwa mapokezi…tunajisikia nyumbani,” alisema.
 Katika ziara yao, ujumbe huo ulitarajiwa  kutembelea maeneo mbalimbali yakiwemo bandari pamoja na kuzungumza na maofisa wa serikali ya Tanzania.
Taarifa za Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), zinaonesha mizigo ya DRC imekuwa ikiongezeka kwa asilimia takribani 24 kwa mwaka tangu mwaka 2004 ikiongezeka kutoka tani 155,611 hadi tani 1,117,249 mwaka 2013.
DRC ni ya pili kwa kupitisha mizigo mingi katika bandari ya Dar es Salaam.  Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, mizigo ya DRC inachukua asilimia 25 ya mizigo yote ya nchi jirani inayopita katika bandari hiyo.

No comments: