TANZANIA, UHOLANZI KUIMARISHA USALAMA SEKTA YA ANGA



Wizara ya Uchukuzi imesaini mkataba na Uholanzi kwa ajili ya kuongeza wigo wa safari za ndege  baina ya nchi  hizo (BASA)  kukabili changamoto za usafiri wa anga  pamoja na kuongeza ulinzi na usalama wa anga.
Mkataba huo ulisainiwa jana Dare s Salaam kati  ya Waziri wa wizara hiyo, Dk Harrison Mwakyembe na Balozi wa Uholanzi nchini,  Jaap Frederiks.
Akizungumza  baada ya kutia saini mkataba huo, Dk Mwakyembe alisema  makubaliano hayo yataweza kutoa fursa nzuri  kwa wasafiri  wa nchi hizo pamoja na mizigo.
Alisema hiyo  ni fursa kwa mashirika mengine  kati ya nchi hizo kujitokeza na kutoa huduma kwa kuongeza idadi ya safari. Pia kutakuwa na ushindani wa nauli pamoja na  kuongeza vituo na kulinda haki za abiria.
Kwa mujibu wa Waziri, ndege zinazofanya safari katika nchi hizo zitatua  katika viwanja vya Songwe na Mwanza tofauti na  awali ambapo walitumia vituo vya  Zanzibar, Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere  (Dar es Salaam) na Mwanza.
Dk Mwakyembe alisema awali  makubaliano kama hayo yaliwahi kufanyika mwaka 1978 ambapo masuala ya anga yalikuwa na upeo mdogo.
 Balozi Jaap alisema soko la Tanzania limekuwa likikua, ikiwa ni pamoja na sekta ya usafiri ambalo ni eneo maalum la kukuza utalii na biashara.

No comments: