KAZI YA KUSAJILI VIZAZI KUFANYWA NA SERIKALI ZA MITAA



Wizara ya Katiba na Sheria imeanza kuboresha kazi ya kusajili vizazi kwa kugatua majukumu hayo kutoka serikali kuu kwenda serikali za mitaa.
Mkakati huo tayari  umeanza  kutekelezwa katika wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam na halmashauri zote za mkoa wa Mbeya. 
Pia, Wizara hiyo imetangaza kuwa inatarajia kuboresha usajili wa vizazi  hadi kufikia asilimia 20 mwakani kutoka asilimia 6.5 za sasa.
Aidha Wizara hiyo imefafanua gharama ambazo Mtanzania, anapaswa kulipa pale anapohitaji cheti cha kuzaliwa, ambapo mtoto au mwombaji ambaye ameandikishwa ndani ya siku 90 tangu azaliwe, gharama ya cheti  hicho ni Sh 3,500 tu.
Kwa mtoto au mwombaji ambaye alichelewa kuandikishwa, yaani baada ya siku 90 tangu azaliwe lakini chini ya miaka 10, gharama ni Sh 4,000; na kwa usajili ya mwombaji aliye na umri zaidi ya miaka 10 tangu kuzaliwa gharama ni Sh 10,000.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Angella Kairuki alisema hayo alipojibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Pauline Gekul (Chadema). Gekul aliuliza “ Je, ni gharama kiasi gani anapaswa kulipa Mtranzania pale anapohitaji cheti cha kuzaliwa?”
Kairuki alisema cheti cha kuzaliwa hutolewa chini ya Sheria ya Uandikishaji wa Vizazi na Vifo Sura ya 108. Sheria hiyo kupitia Tangazo la Serikali Namba 245 la Julai 2000 imeainisha gharama za uandikishaji na utoaji wa cheti cha kuzaliwa. Gharama hizo zinatofautiana kutokana na aina ya kizazi
kinachohitaji kusajiliwa na muda wa kusajili kizazi.
Alisema Wakala wa Usajili, Udhamini na Ufilisi (RITA) umeendelea kuboresha mfumo wa usajili wa vizazi kupitia Mkakati wa Usajili wa Watoto walio chini ya Miaka Mitano (U5BRI) kwa awamu.
“Kupitia mkakati huo serikali imeomdoa gharama ya ada ya cheti kwa toleo la kwanza kwa watoto wenye umri huo kwenye maeneo ambayo mkakati huu umeanza kutekelezwa hususan wilaya ya Temeke na katika halmashauri zote za mkoa wa Mbeya. Halmashauri za mkoa wa Mbeya ni Mbeya, Mbarali, Chunya, Mbozi, Momba, Rungwe, Ileje na  Kyela na Halmashauri ya Jiji la Mbeya.

No comments: