HOJA YA KUMNG'OA SPIKA BUNGE AFRIKA MASHARIKI BADO IKO HAI



Wabunge wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) wamesisitiza kuwa mpango wa  kumng’oa Spika wa Bunge hilo, Margaret Zziwa liko pale pale licha ya wabunge watatu wa Tanzania kuondoa saini zao.
Baada ya Zziwa  kumaliza kusoma sala  na kukaribisha kusomwa kwa bajeti, hatua hiyo haikufanyika kwani baadhi ya wabunge walianza kupiga kelele kulalamika kuwa hakuna ajenda ya kung’olewa kwa spika kwenye shughuli za siku hiyo.
Mbunge Shyrose Bhanji alisimama na kusema   wabunge wa Tanzania akiwemo, Adam Kimbisa,  na Mariamu Ussi wameondoa saini zao katika azimio la kuunga mkono kung’olewa kwa Spika Zziwa madarakani.
Alisema ni kweli Zziwa  ana upungufu  wake lakini mchakato wa kumwondoa madarakani una hatua zake moja baada ya nyingine. Alisema, “sasa nimegundua kuna ajenda ya siri ambayo imezidi yale mapungufu ya spika na ndiyo lengo la kutaka kumuondoa madarakani.”
Bhanji alisema  amejaribu kuelewesha kwamba kama wabunge hao wanataka kwenda na jambo hili si vibaya wakienda nalo hatua kwa hatua ingawa baadhi yao, wanataka lichukuliwe bila utaratibu.
Alisema bunge hilo lilikuwa linatakiwa kusoma Bajeti ya Afrika Mashariki tangu juzi lakini mpaka sasa hivi wabunge wamekataa badala yake, wanataka suala la kung’olewaa spika ndio lipewe kipaumbele.
Aliendelea kusema, “Na utaratibu wa kumuondoa Spika unasema lazima kuwe na saini za wabunge wanne kutoka kila nchi wanachama na kwa sababu hiyo Tanzania saini zimebakia mbili, basi kwa sasa azimio hili limeshakufa halina nguvu tena kisheria.”
 “Nimeliangalia suala hili kwa mapana yake na kuona masuala ya wananchi wa Afrika Mashariki ndio jambo muhimu linalopaswa kupewa kipaumblele na si ajenda hii ambayo pengine kuna ajenda iliyojificha nyuma yake”, alifafanua Bhanji.
Mwanasheria wa EAC na Bunge hilo, Wilbert Kahwa alisema kutolewa kwa saini za wabunge watatu wa Tanzania haina maana kwa sababu saini hizo zilikuwa ni kwa ajili ya kuunga mkono jambo hilo katika hatua za awali kwa ajili ya kutengeneza azimio, sasa azimio tayari limeshatengenezwa  na lipo ndani ya Bunge.
 “Saini hizo 3 haziwezi kuzuia azimio la kumng'oa Spika kwani tayari ilishafika bungeni azimio linaenda mbele halirudi nyuma,” alisema.
Awali wabunge hao kutoka nchi za EAC walikuwa na malalamiko ya kutokuwa na imani na Zziwa na kuazimia kumng'oa. Baadhi ya wabunge wanajitoa  katika msimamo huo ili bajeti ya EAC iweze kupitishwa.

No comments: