Wanafunzi
wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) jana waliandamana kwenda Wizara ya
Sayansi na Teknolojia wakidai hawajaridhishwa na uamuzi wa uongozi wa chuo
kuwazuia wanafunzi 684 kufanya mtihani.
Imeelezwa
kuwa wanafunzi hao hawajaruhusiwa kufanya mtihani kutokana na kushindwa
kukamilisha ada na usajili wa kufanya mtihani uliotakiwa kuanza juzi.
Rais
wa Serikali ya Wanafunzi DIT, Himida Elihuruma alisema hayo jana, Dar es
Salaaam wakati wa maandamano hayo. Alisema utaratibu wa kujisajili uliowekwa na
taasisi hiyo haujafuatwa hivyo kuleta mkanganyiko kwa wanafunzi hao kujua siku
ya kukamilisha usajili.
Alisema
wapo wanafunzi waliokamilisha usajili, lakini wamewekwa katika idadi ya ambao
hawajakamilisha hatua hiyo, na hali hiyo imetokana na utaratibu mbovu wa
kutunza kumbukumbu za wanafunzi.
“Sisi
tumeandamana kupinga uamuzi wa mkuu wa chuo kwani kila mwanafunzi ana haki ya
kufanya mtihani kulingana na utaratibu
wa chuo, wasiolipa ada wanapaswa kuzuiwa wasichukue matokeo kama mwaka jana,
’’alisema Elihuruma.
Naye,
Ofisa Uhusiano wa DIT, Amani Kakana alisema idadi kamili ya wanafunzi
wasiosajiliwa ni 180 na sio idadi iliyotajwa na serikali ya wanafunzi.
Alisema
uongozi haujachukua hatua zaidi ya kuwataka kuendelea na mitihani kwa wenye
vigezo.
Alisema
kundi la watu wachache ndio limewachochea wanafunzi wengine kuingia katika
mgomo huo na wakati wenzao wanafanya mtihani walifanya vurugu kwa kuwatoa
katika chumba cha mtihani huo.
Katibu
Mkuu Wizara ya Sayansi na Teknolojia, Patrick Makungu aliwasisitiza wanafunzi
hao kurudi chuoni hapo kwani matatizo yao yatatatuliwa kama walivyotarajia.
No comments:
Post a Comment