TIBA ASILI WANAODAI KUTIBU UKIMWI SASA KUKAMATWA



Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imeagiza vyombo vya dola, kukamata waganga wa jadi, wanaojitangaza kutibu magonjwa ya Ukimwi, kisukari na shinikizo la damu.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii,
Dk Seif Rashid alipokuwa akiwasilisha bungeni hotuba ya  bajeti ya Wizara yake kwa mwaka wa fedha 2014/15.
Aliwasihi wataalamu wa tiba asili na tiba mbadala, kuacha mara moja, kujitangaza kuwa na uwezo wa kutoa tiba dhidi ya  ugonjwa wowote ule ambao uwezo huo haujathibitishwa kitaalamu.
“Hilo ni kosa kwa mujibu wa sheria iliyoanzisha tiba asili na tiba mbadala,” alisema.
Waziri huyo alisema yapo matangazo yanayohusu kuwa na uwezo wa kutibu Ukimwi, kisukari na shinikizo la damu. “Kwa mujibu wa Sheria ya Tiba asili na Tiba mbadala, matangazo hayo yaondolewe mara moja,” alisema.
Alieleza kuwa wizara itatoa mwongozo na taratibu zinazopaswa kufuatwa ili dawa husika zithibitishwe kitaalamu.
 “Napenda kuchukua fursa hii kuagiza vyombo husika vya serikali, vifuatilie kwa karibu na kuchukua hatua kwa mujibu wa sheriakwa wale watakaokwenda kinyume na sheria,” alisema.
Waziri huyo pia alizungumzia suala la tiba za kibingwa, ili
kupunguza idadi ya wagonjwa  wanaokwenda nje ya nchi kwa uchunguzi na matibabu.
Alisema Wizara inaendelea kuanzisha huduma za tiba za kibingwa katika hospitali za Kanda, hospitali Maalum na Hospitali ya Taifa Muhimbili ili kupunguzwa wagonjwa hao wa kwenda nje ya nchi.
Alisema huduma za upasuaji mkubwa wa moyo, zimeendelea kutolewa ambapo hadi sasa wagonjwa 671 walipata huduma hiyo kwa mafanikio katika hospitali za Muhimbili, Bungando na KCMC.
Aidha, wagonjwa 211 walifanyiwa upasuaji maalum katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), ambapo 29 walifanyiwa upasuaji wa ubongo,  107 upasuaji wa uti wa mgongo, 56 waliwekewa viungo bandia vya nyonga na 19 viungo bandia vya goti.
Dk Rashid alisema katika mwaka 2014/15 Taasisi ya Mifupa Muhimbili  inatarajia kuwahudumia wagonjwa wapatao 6,900.
Aidha, itafanya upasuaji wa kuweka viungo bandia vya nyonga kwa wagonjwa 400, kuweka viungo bandia vya goti kwa wagonjwa 150, upasuaji wa ubongo kwa wagonjwa 240, upasuaji wa uti wa mgongo na mishipa ya fahamu kwa wagonjwa 400 na upasuaji wa watoto wenye vichwa vikubwa 600.
Bajeti aliyoomba ili kuiwezesha Wizara yake kutekelezwa kazi zilizopangwa katika mwaka 2014/15, Waziri huyo aliomba Bunge  kuidhinisha  makadirio  ya matumizi ya wizara hiyo pamoja na taasisi zake yenye Sh bilioni 622.95, ambapo kati ya hizo Sh bilioni 317.22 ni kwa ajili ya matumizi ya kwaida na Sh bilioni 305.72 ni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

No comments: