BABA WA 'MTOTO WA BOKSI' AKWAMA KUMZIKA MWANAWE



Safari ya mwisho ya mtoto Nasra Mvungi (4), iliyokuwa ya mateso hapa duniani, imefikia mwisho jana katika makaburi ya Kola, Manispaa ya Morogoro, bila kusindikizwa na baba yake mzazi, Rashid Mvungi.
Nasra kwa zaidi ya miaka mitatu hapa duniani, inadaiwa alikuwa akiishi katika boksi lililokuwa kitanda, choo, sehemu ya kuchezea na meza yake ya kulia chakula.
Mvungi alishiriki kwenda jijini Dar es Salaam kuchukua mwili wa mwanawe, na hata jana wakati wa kutoa mwili katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kwenda kumwosha msikitini, alikuwepo.
Baada ya hapo mwili ulipelekwa uwanja wa Jamuhuri, ambako Mvungi wakati wote alikuwa ameketi mstari wa mbele ya jeneza la mwanawe. Uwanjani hapo nasaha mbalimbali za viongozi wa Serikali na wale wa dini zilitolewa mbele yake.
Baada ya nasaha za viongozi wa Serikali na dini kumalizika, huku zingine zikimlenga Mvungi moja kwa moja, mwili wa Nasra ulichukuliwa na kurejeshwa msikitini kwa ajili ya kuswaliwa, huku Mvungi akichukuliwa na askari Polisi wa Kitengo cha Upelelezi Mkoa.
Kutokana na hatua hiyo, baada ya swala mwili wa Nasra ulipelekwa katika makaburi ya Kola kwa hatua za mwisho za maziko, bila uwepo wa Mvungi.
Akizungumza na mwandishi makaburini kuhusu sababu za kutohudhuria kwa Mvungi makaburini, Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Mkoa, Japhet Kibona, alisema isingekuwa   busara kumruhusu baba huyo ashiriki maziko makaburini kutokana na hasira za wananchi.
Hata Kaimu Shekhe wa Mkoa wa Morogoro, Ally Omar, alipokuwa akitangaza utaratibu wa kuweka udongo kaburini, ambao kwa kawaida hutaja majina ya wahusika wakuu, Mvungi hakuwa miongoni mwa waliotarajiwa kumsindikiza Nasra. 
Badala yake katika orodha hiyo ya waliotakiwa kuweka udongo kaburini, Shekhe Omar alimwita Mkuu wa Mkoa, Joel Bendera,  Mbunge wa Morogoro Mjini, Abdulaziz Abood na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Mkoa, Kibona, ambaye alimwakilisha Kamanda wa Polisi wa Mkoa.
Wengine waliopata fursa ya kuweka udongo katika kaburi hilo ni Ofisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Morogoro, Oswin Ngungamtitu na Mkurugenzi wa Kampuni ya Mabasi ya Al –Saed, Omary Al- Saed, ambaye alijitolea gharama za kusafirisha mwili wa Nasra kutoka Hospitali ya Taifa  Muhimbili jijini Dar es Salaam na za mazishi yake.
Ingawa tayari Mvungi anakabiliwa na mashitaka ya kula njama na kufanya ukatili dhidi ya mtoto huyo, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mjini Morogoro, viongozi waliotoa nasaha katika uwanja wa Jamuhuri, walijikuta wakishindwa kuacha kumtaja baba huyo.
Alianza Mkuu Mkoa, Bendera alisema mateso aliyopata Nasra   kwa kufungiwa kwenye boksi kwa zaidi ya miaka mitatu, ni unyama na umetia aibu Mkoa wa Morogoro.
Alisema kuwa kitendo hicho si cha kufurahisha kwa binadamu yeyote aliyeumbwa na Mwenyezi Mungu na aliye na dini. “Unamweka mtoto ndani ya boksi kwa miaka mitatu wakati wewe unanenepeana na unakuwa na amani? Jamani tuwe na uoga na Mwenyezi Mungu.”
Aliwataka viongozi wa serikali za mitaa na vijiji kujenga utamaduni wa kutembelea nyumba zote, ili kujua watu wote wanaoishi na kuongeza kwamba kungekuwa na utamaduni huo tangu awali, mtoto Nasra asingefanyiwa ukatili huo.
Pia alikemea vitendo vya wazazi wa kiume kutelekeza watoto wao: “Haiwezekani unamzaa mtoto halafu unamtelekeza… nakuhakikishia Mvungi adhabu utaibeba.”
Baada ya Bendera, Mbunge wa Morogoro, Aziz Abood alisema kitendo kilichofanywa na walezi wa Nasra si cha kiungwana na kumetia aibu Mkoa wa Morogoro.
Abood alisema amekuwa akipata shida kutoka kwa wabunge wenzake waliokuwa bungeni, kutokana na kitengo hicho ambapo   wengi wamekuwa wakihoji kuhusu ukatili aliofanyiwa mtoto huyo.
“Nimekuwa nikiulizwa kulikoni mkoani Morogoro mmenza kufungia watoto ndani ya boksi?“Alisema Abood.
Mbunge huyo aliahidi kushirikiana Mkuu wa Mkoa kuhakikisha sheria inachukuwa mkondo wake kwa wote waliohusika na ukatili huo na kuongeza kuwa endapo wahusika watatoka kwa njia za panya, watarudishwa tena ndani.

Pia aliahidi kumfanyia hitima ya mwisho mtoto huyo, ambayo
inatarajiwa kufanyika katika uwanja huo huo wa Jamhuri.
Shekhe Omari alisema ana mashaka na Uislamu wa  wahusika wanaotuhumiwa kwa ukatili kwa mtoto huyo, kwa kuwa ni kinyume si tu cha sheria, bali pia  na maadili ya dini hiyo kwa kuwa Uisilamu unafundisha upendo.
Alitaka sheria iangaliwe hata kwa wale majirani wa mama mlezi wa mtoto huyo, ambao alisema kama wangetoa taarifa mapema yasingetokea hayo yaliyotokea kwa mtoto Nasra.
“Majirani waliokuwa wanaishi na yule mama aliyekuwa anamtesa matoto wanachukuliwa hatua gani?” Alihoji Shekhe Omari.
Alisema kuwa tendo hilo linaonekana kuwa na imani za kishirikina ndani yake, kwa kuwa katika hali ya kawaida haiwezekani mtu amfungie mtoto ndani ya boksi huku akiwa anajisaidia humo na ukaridhika na harufu.

No comments: