Watoto
wanaozaliwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma wakiwa na ugonjwa wa homa ya
njano, inasadikiwa wamekuwa wakianikwa juani kutokana na ukosefu wa mashine
maalumu ya kufanya kazi hiyo.
Hata
hivyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Hospitali hiyo ya Rufaa ya Mkoa, Balozi Job
Lusinde amesema hali hiyo haitajitokeza tena kutokana na hospitali hiyo
kupatiwa msaada wa mashine ya kisasa ya matibabu kwa njia ya mionzi.
Mashine
hiyo ilitolewa na benki ya CRDB wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa
Afrika, yaliyofanyika mjini hapa.
“Watoto
walikuwa wakianikwa juani kama pumba ili kuwanusuru madhara ya ugonjwa huo,
tunaishukuru sana CRDB kwani mashine hii itasaidia uhai wa watoto wengi,”
alisema.
Daktari
Bingwa wa uzazi na wanawake Enid Chiwanga alisema wanatumia njia ya kuanika
watoto wachanga juani wanapozaliwa na homa ya manjano kutokana na kukosekana
kwa mashine.
“Watoto
wanapozaliwa tulikuwa tukitumia njia ya asili kwa kuwaanika juani wakati
wa asubuhi ili wapate mwanga wa jua,” alisema.
Alisema
msaada huo utaokoa watoto wengi wanaozaliwa na manjano ambayo husababisha
nyongo kuenea mwilini na kusababisha mwili kuwa wa njano hali inayosababisha
pia matatizo ya ubongo.
Mkurugenzi
wa CRDB Tawi la Dodoma, Rehema Hamisi, alisema kwa kutambua umuhimu wa afya ya
mtoto, wameamua kutoa mashine hiyo baada ya kubaini ukosefu wa kifaa hicho
hospitalini hapo.
Kwa
mujibu wa Mkurugenzi huyo wa benki, mwaka 2010, CRDB ilikarabati wadi ya
akinamama na watoto ya hospitali hiyo pamoja na kutoa vitanda 50, magodoro na
mashuka.
Pia
mwaka juzi, benki hiyo ilidhamini mashindano ya Kiswahili mkoani Dodoma
kuongeza ari ya vijana kujifunza lugha ya taifa.
No comments:
Post a Comment