JAPAN YASAIDIA SHILINGI BILIONI 24.1 ZA BAJETI



Serikali ya Tanzania imepata mkopo wa Sh bilioni 24.1 kutoka Serikali ya Japan ikiwa ni sehemu ya kuisaidia bajeti yake.
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum na Balozi wa Japan nchini, Masaki Okanda walitia saini mkataba  wa mkopo huo. Salum alisema fedha hizo zitasaidia katika maeneo muhimu ikiwemo afya, maji na nishati.
Mkuya alisema fedha hizo kwa kiasi kikubwa zitatumika katika kupambana na umasikini.
Alisema juhudi kama hizo zimeimarisha huduma muhimu kwa jamii na kupunguza umaskini katika maeneo mengi ambapo kulingana na ripoti ya sensa ya watu na makazi iliyotolewa hivi karibuni, kiwango cha umasikini kwa Watanzania kimepungua na kipato cha Mtanzania kinapanda.
Kwa upande wake, Balozi wa Japan nchini, Okada alisema mkataba huo ni wa  ushirikiano wa pamoja na Benki ya Dunia na kwa masharti nafuu ya riba ya asilimia 0.01.
Alisema msaada huo hutolewa kulingana na bajeti ya serikali na fedha hizo hulenga utekelezaji wa juhudi za kupunguza umasikini zinazofanywa na serikali ya Tanzania, hususan Mpango wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (Mkukuta).
Balozi huyo alisema serikali ya Japan iko tayari kuongeza msaada kwa Tanzania kufikia malengo ya kuchangia maendeleo ya miundombinu ya barabara, reli, nishati na viwanda.

No comments: