Serikali imesisitiza kufuta baadhi ya hati
miliki za mashamba ya mkonge katika Mkoa wa Tanga na kugawia wananchi.
Waziri
wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza, aliliambia Bunge jana
kuwa tayari baadhi ya mashamba yamepelekwa Ofisi ya Rais kwa ajili ya kufutiwa
hati miliki.
Chiza
pia alisema wakulima wengi wameshindwa kuendeleza mashamba hayo kutokana na
kuwapo migogoro kwa wamiliki kutumia mashamba hayo kujipatia mikopo kutoka
kwenye benki.
Akitoa
mfano wa utekelezaji wa hilo, Chiza alisema kuwa serikali imefanikiwa kurejesha
mashamba ya Pongwe, na tayari ardhi hiyo imepimwa na kugawiwa kwa wananchi.
“Tunawafuatilia
wawekezaji wengine katika sekta ya mkonge ili tujue changamoto zinazowakabili
kabla ya kuwanyang’anya na kuwatafuta wawekezaji wengine kwa ajili ya
kuendeleza mashamba,” alisema.
Alisema
kuna baadhi ya wawekezaji ambao wamechukua mikopo benki kwa kutumia mashamba
kama udhamini na wameshindwa kulipa mikopo hiyo, jambo ambalo limelazimisha
benki kushikilia hati miliki.
Chiza
alielezea uamuzi wa kubinafsisha mashamba makubwa ulifikiwa na serikali kati ya
mwaka 1996 na 1999 na kutekelezwa na Tume ya Kurekebisha Mashirika ya Sekta ya
Umma (PSRC).
Alisema
lengo lilikuwa ni kuinua uzalishaji, lakini baadhi yao wameshindwa na kutolea
mfano mashamba ya Marungu, Pongwe, Amboni na Kilimangwido.
Chiza
alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Amina Mohamed Mwidau (CUF)
aliyetaka kujua Serikali ina mpango gani na mashamba ya mkonge katika Wilaya ya
Tanga na Pangani ambayo hayazalishi tena.
No comments:
Post a Comment