WAASWA KUNUNUA VIFAA IMARA VYA BODABODA



Waendesha pikipiki, maarufu ‘Bodaboda’ wameshauriwa kununua vifaa sahihi kwa ajili ya vyombo hivyo ili kuepuka madhara yanayoweza kuwatokea pindi wakitoa huduma ya usafiri.
Ushauri huo ulitolewa jana jijini hapa na Meneja Masoko, Kanda ya Afrika kutoka Kampuni ya Mek-one General Traders, Benard Kituyi wakati akitambulisha mafuta ya Shell Advance mahususi kwa pikipiki.
Alisema baadhi ya wamiliki na madereva wa bodaboda hushindwa kununua vifaa sahihi kwa ajili ya pikipiki zao jambo ambalo husababisha wakati mwingine kutokea tatizo ambalo lingeweza kudhibitiwa mapema.
“Unapotumia vifaa ambavyo si mahususi kwa pikipiki ni wazi kwamba unafanya usafiri husika kupokea kitu ambacho si sahihi kwake na hivyo kulazimisha jambo ambalo ni hatari kwa vifaa vya moto,”alisema Katuyi.
Alisema katika kuhakikisha huduma ya usafiri wa pikipiki inakuwa salama, kampuni hiyo ina mpango wa kukutana na waendesha bodaboda 30,000 ambao watawaelimisha umuhimu wa kutumia mafuta hayo na namna ya kutumia barabara kwa njia salama.
“Mafunzo hayo yatatolewa kwa wiki moja kuanzia leo (jana) yakiambatana na kutoa vifaa kama makoti maalum ‘reflect jacket’ ya kuvaa ambayo yatawasaidia kuonekana wawapo barabarani, hivyo kuwakinga na ajali,” alisema.
Alisema kwa kuanzia mafunzo hayo yataanzia Dar es Salaam yakifuatiwa na Arusha, Mbeya na mikoa mingine ambayo wanaamini usafiri huo unatumiwa kwa wingi na watu.
Kwa upande wake mmoja wa waendesha bodaboda, Razaki Juma, alizishukuru kampuni hizo kwa kujitoa kuwapa  elimu ya namna ya kutumia mafuta kwani awali walikuwa hawajui matumizi ya mafuta ya magari kama ndio yanachangia kila siku kupeleka pikipiki zao kwa mafundi.

No comments: