Chama cha Wasioona Tanzania (TLB)
Manispaa ya Dodoma wamewaomba wasamaria kuwasaidia kupata fimbo nyeupe zitakazowatambulisha.
Mratibu wa mradi wa Ulingo wa
majadiliano kuhusu uwezeshwaji, ujumuishwaji na utetezi wa mahitaji na haki za
wenye ulemavu wa macho Mathias Fyejeje
amesema ukosefu wa fimbo hizo unawaweka rehani walemavu hao.
Mratibu huyo alisema hayo katika
mkutano wa ulingo uliofanyika Miyuji, Dodoma.
Fyejeje alisema tatizo hilo la ukosefu
wa fimbo nyeupe kwa wasioona ni tatizo hasa wanapokuwa karibu na barabara kwani
madereva hawawezi kutambua kwamba alio mbele yao ni mtu asiyeona.
Alisema kazi kubwa ya fimbo hizo nyeupe
ni kumtambulisha asiyeona anapokuwa barabarani kwa madereva na watembea kwa
miguu kwani anakuwa hawezi kukwepa hatari yoyote bali huyo anayeona anapaswa
kufanya hivyo kutokana na kuiona fimbo hiyo.
Mratibu huyo alisema wanahitaji fimbo 150 kutokana na idadi
ya wasioona waliopo katika chama hicho cha wilaya ambazo kila moja inauzwa kati
ya 30,000 na 35,000 na hivi sasa wamekwishapokea fimbo 40 toka kwa wahisani
mbalimbali na hivyo kusaliwa na 110.
Aidha aliongeza kuwa miundombinu kwa
wasioona ni tatizo hasa kwa majengo na barabara ambapo ameshauri ngazi zote za
majengo ziwe na vizuizi vya pembeni, mifereji Êna madaraja yawekewe tahadhari
ya watu wenye ulemavu huo.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya
Mnadani Manispaa ya Dodoma Stiven Masangia aliyefungua ulingo huo wa
majadiliano aliwataka wahisani mbalimbali kuwanunulia fimbo hizo na Serikali
kuwajengea miundombinu rafiki ili kuepusha ajali zisizo za lazima kwa wasioona.
No comments:
Post a Comment