Watu wawili wanaosadikiwa kuwa ni
majambazi wakiwa na silaha aina ya shortgun
wamepora kiasi cha Sh milioni 20 kutoka
kwa mtumishi wa duka la kubadilishia fedha za kigeni la Northern Bureua de
Change na kumpiga risasi mtu mmoja na kufa hapo hapo.
Tukio hilo lililotokea saa 3.30 asubuhi
jana katika duka hilo mali ya Hotel ya Impala lililopo mtaa wa Maeda katikati
ya Jiji la Arusha. Watuhumiwa hao wakiwa na pikipiki waliondoka eneo hilo
kupitia barabara ya zamani ya Moshi kuelekea Kijenge mara baada ya tukio hilo.
Kwa mujibu wa watu walioshuhudia tukio
hilo, walisema majambazi hao walifika eneo hilo pikipiki na kuegesha eneo
zinapoegeshwa teksi na kumsubiri mtumishi wa duka hilo aliyetambuliwa kwa jina
moja la mama Msuya ambaye jana aliingia kazini na usafiri mwingine tofauti na
unaojulikana.
Mmoja wa watu hao ambaye hakuwa tayari
kusema jina lake, aliendelea kusema mara baada mtumishi huyo kufika akiwa na
mfuko mweusi wenye kiasi hicho cha fedha, ghafla alivamiwa mlangoni wakati
akiwa anafungua duka hilo na kuanza kunyang'anyana mfuko huo.
Alisema wakati jambazi huyo mmoja
akipambana na mama Msuya na kumpiga kibao huku akimuamurisha kutoa fuko hilo la
fedha, mama huyo alipiga kelele kuomba msaada na madereza teksi walikwenda
ghafla kutaka kumsaidia.
Lakini hali ilibadilika baada ya
jambazi mwingine aliyebaki katika pikipiki kutelemka na silaha na kwenda
kumpiga risasi mmoja wa watu aliyetaka kwenda kutoa msaada aliyetambuliwa kwa
jina mmoja la Mmasi ambaye ni mchimba madini ya tanzanite na kufa hapo hapo.
Mtoa habari huyo alisema marehemu
alikuwa ametoka kusali katika kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT)
usharika wa mjini kati na alikwenda kununua magazeti eneo hilo hilo na alipoona mama akipiga kelele kuomba msaada,
alikwenda kwa lengo kumukoa lakini kabla ya kufika alipigwa risasi ubavuni na kufa hapo hapo na jambazi
aliyekuwa pembeni na toyo.
No comments:
Post a Comment