SHILINGI BILIONI 7 ZATENGWA KUKABILI KERO YA MAJI DAR



Serikali imetenga Sh bilioni saba katika mwaka wa fedha 2014/15, kwa ajili ya  kulipa fidia kwa wananchi ili kupisha mradi wa bwawa la Kidunda, litakalotumika kukabili adha ya maji jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe alisema juzi kuwa Mthamini wa Serikali amekamilisha kazi yake ambayo imeongeza thamani ya fidia kutokana na kuchelewa malipo.
Profesa Maghembe alisema kulingana na Sheria ya Ardhi Namba 4 ya mwaka 1999, thamani ya fidia imeongezeka kwa asilimia nane.
"Vitabu vipya vimetayarishwa na rasimu ziliwasilishwa Februari 28, 2014. Taratibu za kupata fedha za kulipia fidia hiyo ambayo ni shilingi bilioni 7.9 zinaendelea.
"Katika mwaka 2014/2015, Serikali imepanga kutumia Shilingi bilioni saba kwa ajili ya maandalizi na ulipaji fidia," alisema Profesa Maghembe wakati akiwasilisha bungeni bajeti yake ya 2014/15.
Alisema Wizara inaendelea na juhudi za kutafuta fedha za ujenzi wa bwawa hilo na hivi sasa yapo mashauriano kati ya Benki ya Uwekezaji ya Afrika Kusini, ikishirikiana na Benki ya Rasilimali Tanzania, na Benki ya Dunia, kwa ajili ya kupata fedha za ujenzi huo.
Ujenzi wa bwawa la Kidunda ni moja ya miradi ya kukabili tatizo la maji katika Jiji la Dar es Salaam. Waziri alisema ujenzi utaanza katika mwaka wa 2014/15.
Aidha, alisema miradi mingine ya kuipatia maji Jiji la Dar es Salaam inaendelea ambayo ni pamoja na visima virefu vya Kimbiji na Mpera, upanuzi wa mtambo wa Ruvu Juu na Ruvu Chini na ukarabati na upanuzi wa mfumo wa kusambaza majisafi.
Alisema ulazaji wa bomba kuu kutoka Mlandizi hadi Kimara umeanza Februari 15, mwaka huu, na mradi huu unatarajiwa kukamilika baada ya miezi 18.
Kuhusu mradi wa Ruvu Chini, alisema hadi Machi mwaka huu, kazi ya ulazaji bomba kuu kutoka mitambo ya Ruvu Chini hadi matangi ya Chuo Kikuu cha Ardhi lenye urefu wa kilometa 55.93, umekamilika kwa asilimia 62.87, sawa na kilometa 35.16.
Kuhusu miradi ya maji ya miji midogo nchini, Profesa Maghembe alisema Serikali imetenga Sh bilioni 17.1 kwa ajili ya kukarabati na kupanua miundombinu ya maji katika miji mikuu ya wilaya na miji midogo 46.
"Fedha hizo zitatumika kutekeleza miradi inayoendelea na ambayo italeta ahueni kubwa ya maji kwa wakazi wa miji hiyo," alisema Profesa Maghembe.
Wizara ya Maji imeomba kuidhinishiwa Sh 520,906,475,000 kwa ajili ya matumizi ya wizara, ambazo kati ya hizo, Sh 30,899,443,000 zikiwa ni za matumizi ya kawaida, sawa na asilimia sita ya bajeti na asilimia 94 zitakuwa kwa ajii ya maendeleo.

No comments: