MAMA MZAZI WA ZITTO KABWE AFARIKI DUNIA KWA SARATANI



Mama mzazi wa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto, Shida Salum, amefariki dunia baada ya kusumbuliwa kwa muda mrefu na maradhi ya saratani.
Akizungumza na mwandishi, Dar es Salaam jana, mtoto wa kwanza wa mama huyo ambaye pia alikuwa ni Mwenyekiti wa Chama cha Walemavu Tanzania, (Chawata), Salum alisema, mama yake alifariki majira ya saa tano asubuhi jana katika hospitali ya Ami, Masaki, Dar es Salaam.
"Ni kweli mama yetu mpendwa ametutoka saa tano asubuhi hii leo (jana), akiwa hospitalini akipatiwa matibabu, tunamsafirisha leo (jana) kwenda Kigoma kwa maziko," alisema.
Alisema kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa, Shida ambaye pia alikuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), atazikwa leo saa tisa alasiri Kigoma mjini.
Mwandishi, alijaribu kuwatafuta wasemaji wa Chadema ambao ni Tumaini Makene na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa Chadema, John Mnyika bila mafanikio, baada ya simu zao kuita bila kupokelewa huku nyingine zikiwa zimezimwa.
Hata hivyo, katika ukurasa wake kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook, Tumaini, aliandika "Mwenyezi Mungu amlaze mahali pema Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, marehemu Shida Salum,"
Alimuomba Mungu awatie nguvu na moyo wa subira wakati huu wa majonzi mazito wafiwa, kipekee zaidi familia na wajumbe wenzake wa Kamati Kuu ya Chadema kwa kuondokewa na mpendwa wao huyo.
Shida, ameacha watoto 10 akiwemo Zitto ambaye naye kwa sasa amekuwa akiandamwa na matatizo ya kisiasa wakati akikabiliwa na tatizo la kumuuguza mama yake.

No comments: