LAPF WAWEKA KIWANGO CHA MISAADA KWA JAMII



Mfuko wa Pensheni LAPF umesema kuanzia sasa misaada ya kijamii  itakayotolewa na mfuko huo utakuwa ni kati ya Sh 500,000 na Sh milioni tatu.
Uamuzi huo unatokana na mfuko huo kupokea maombi mengi, wakati bajeti yake ya misaada kwa jamii ni Sh milioni 130.
"Kutokana na ufinyu wa bajeti na maombi kuwa mengi sehemu kubwa ya misaada inayotolewa ni kati ya Sh 500,000 hadi Sh milioni tatu," haya yamo kwenye taarifa ya mfuko iliyotolewa kwa vyombo vya habari.
LAPF  imesisitiza kwamba kusaidia jamii ni utaratibu wake wa kawaida na ni sehemu ya vigezo vya utawala bora. Mfuko huo umefafanua kuwa misaada hiyo hutolewa moja kwa moja kwa walengwa na si kwa kutoa fedha taslimu, bali kwa kununua vifaa husika.
Taarifa hiyo pamoja na masuala mengine, ililenga pia kukanusha kukopesha baadhi ya wabunge kama ambavyo taarifa zilivyotolewa na baadhi ya vyombo vya habari hivi karibuni.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, mfuko huo umesema pamoja na kuandikisha wanachama, kukusanya michango, uwekezaji na kulipa mafao, mfuko huo unashiriki pia katika kusaidia jamii na hivyo kusaidia katika kupunguza umasikini na kuchochea maendeleo.
"Utaratibu huu ni wa kawaida kwa taasisi zote za hifadhi ya jamii pamoja na taasisi nyingine za umma na taasisi za binafsi hapa nchini. Utoaji wa misaada ya kijamii ni sehemu ya vigezo vya utawala bora," ilisema taarifa ya LAPF.
Ilielezwa kuwa LAPF imekuwa ikitoa misaada ya kijamii katika sekta mbalimbali kama vile afya, elimu, vituo vya kulelea watoto yatima, taasisi za watu wenye mahitaji maalumu, sekta ya michezo na kusaidia katika matukio ya maafa.
Katika sekta ya afya, matukio ya maafa na vituo vya kulelea watoto yatima, LAPF imesema imekuwa ikitoa msaada wa chakula na vifaa mbalimbali kama vyandarua, magodoro, shuka, dawa na vifaa vya maabara.
Kwa upande wa sekta ya elimu mfuko umekuwa ukichangia madawati, mabati, saruji, taa zinazotumia nguvu ya jua na mashine za kudurufu nyaraka. Aidha katika michezo, unachangia vifaa mbalimbali vile kama vile mipira na jezi.

No comments: