Katika mwaka wa fedha 2014/15
Serikali itakuwa inatangaza watu wanaonufaika na misamaha ya kodi.
Lengo la hatua hiyo ni kuongeza haki
na usawa katika kutoa misamaha hiyo.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa
Fedha, Saada Mkuya Salum kwenye Hotuba yake ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka
2014/15.
“Sambamba na kupunguza misamaha ya
kodi na kuongeza haki na usawa katika kutoa misamaha, kuanzia mwaka 2014/15
serikali itachukua hatua kuu mbili muhimu”, alisema.
Saada alisema hatua ya kwanza
itakayochukuliwa ni Serikali itakuwa inatoa taarifa ya misamaha ya kodi kila
robo mwaka, kwa kuwatangaza walionufaika na misamaha kwenye tovuti ya
Wizara ya Fedha.
Taarifa hiyo itajumuisha majina ya
watu, taasisi, asasi na kampuni zilizonufaika na misamaha ya kodi,
thamani na sheria iliyotumika kutoa misamaha hiyo.
Alieleza kuwa zoezi hilo,
litahusisha taarifa ya misamaha ya kodi
ya kuanzia mwaka 2010 na kuendelea.
“Hatua hii itasaidia kuleta uwazi na
uwajibikaji katika suala la misamaha ya kodi na kuwafanya wananchi wajue ni
nani anayenufaika na misamaha hiyo,” alisema.
Alisema, hatua ya pili
itakayochukuliwa ni kutoa taarifa ya kina ya misamaha yote ya kodi iliyotolewa
na kuiwasilisha bungeni kila mwaka ili wabunge wapate nafasi ya kujadili na
kutoa maoni yao.
No comments:
Post a Comment