Serikali imepokea Sh bilioni 127
kutoka TIPER ikiwa ni gawio ambalo kampuni hiyo imekuwa ikilipa kwa wanahisa
wake kila mwaka.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu
Wizara ya Fedha, Dk Servarcius Likwelile alipokuwa akipokea gawio hilo katika
hafla iliyofanyika jana mjini Dodoma.
Dk Likwelile alisema kuwa gawio hilo
litaelekezwa kwenye bajeti ya mwaka huu wa fedha 2013/14 unaomalizika kwa
kuangalia maeneo ambayo yanawagusa wananchi ikiwemo sekta ya elimu, afya na
maji.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji
wa kampuni hiyo, Daniel Belair alisema kuwa si mara ya kwanza kwa kampuni yake
kutoa gawio kama hilo kwa Serikali ambapo mwaka jana muda kama huu kampuni
ilitoa kiasi kama hicho kama gawio.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa kampuni
yake imeendelea kufanya vizuri katika kukuza maisha ya kijamii na kiuchumi
ambapo kwa sasa inafanyakazi kwa saa 24 na siku saba za wiki.
Kwa kuzingatia utendaji huo, Kampuni
ya TIPER imekuwa kichocheo kikuu cha kuzalisha ajira nchini ambapo hadi sasa
asilimia 99 ya wafanyakazi wake ni nguvu kazi ya Watanzania.
Naye Mwenyekiti Mtendaji wa Bodi ya
Wakurugenzi ya TIPER, Profesa Abdulkarim Mruma alisema kuwa imekuwa ni muhimu
kwa kampuni yao kuwa na akiba ya kutosha ya mafuta kwa nchi na kuleta mafanikio
makubwa ya upatikanaji wa mafuta nchini.
Aidha, TIPER Profesa Mruma alisema
kuwa kwa sasa kampuni yao imejikita katika kuleta mafuta yaliyosafishwa nchini
ili kupunguza gharama zisizokuwa za lazima.
“Kwa sasa tunaleta mafuta
yaliyosafishwa badala ya mafuta ghafi ambayo yanazalisha tope jingi ambalo
limekuwa ni hatari katika kutunza mazingira yetu,” alisema Profesa Mruma.
Pamoja na ufanisi huo, kumekuwepo na
changamoto za kuboresha mkataba wa utendaji na usimamizi wa hesabu masuala
ambayo wanahisa wote wawili wanaendelea kuyafanyia kazi kwa madhumuni ya kuwa
na matokeo mazuri zaidi kwa pande zote.
Kiutendaji Kampuni ya TIPER
inaendeshwa kwa ubia kati ya Serikali ya Tanzania ambayo ina hisa zenye
asilimia 50 na Kampuni ya Oryx Energies SA asilimia 50.
Pamoja na Tanzania, Kampuni ya Oryx
Energies SA inafanya kazi katika nchi mbalimbali duniani ambazo ni Benin,
Burkina Faso, Côte d'Ivoire, Guinea Conakry, Kenya, Mali, Niger, Nigeria,
Senegal, Sierra Leone, Afrika Kusini, Uhispania (Visiwa vya Canary),
Togo, Uganda na Zambia.
No comments:
Post a Comment