WAWAKILISHI WAKERWA KUPAPASWA UWANJA WA NDEGE



Baadhi ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wameitaka Wizara ya Mawasiliano na Miundombinu kuweka vifaa vya kisasa vya ukaguzi kwa abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar na kuacha tabia ya kuwakagua abiria kwa kuwapapasa mwili.
Mwanajuma Faki Mdachi, Mwakilishi wa Viti Maalumu kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF), akichangia bajeti hiyo alisema anakerwa na tabia ya kupapaswa mwilini inayofanywa na wafanyakazi wa uwanja wa ndege wakati abiria wanapoondoka nchini.
Alisema haipendezi hata kidogo kuona abiria wanapapaswa mwilini wakati wa kufanya ukaguzi badala ya kutumia vifaa vya kisasa kama ilivyo kwa nchi nyingine.
“Mheshimiwa Spika tunaitaka Wizara ya Mawasiliano na Miundombinu kutafuta vifaa vya kisasa vya kufanya ukaguzi wa abiria na mizigo na kuacha tabia ya kutupapasa mwilini...hii si tabia nzuri hata kidogo,” alisema.
Alisema wakati mwingine mwanamume hufanya ukaguzi kwa kuwapekua abiria wanawake kitendo ambacho hakikubaliki hata kidogo kwani huo ni sawa na udhalilishaji wa kijinsia.
Naye Mwakilishi wa Jimbo la Chake Chake kwa tiketi ya CUF, Omar Ali Shehe aliitaka mamlaka ya viwanja vya ndege vya Zanzibar kutafuta vifaa vya kisasa vyenye uwezo wa kugundua vitu mbali mbali ikiwemo madawa ya kulevya.
Alisema kwa sasa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amaan Karume hauna vifaa vya kisasa vya kufanya ukaguzi ambapo wafanyakazi wake wanalazimika kuwapapasa abiria.
“Mheshimiwa Spika wakati umefika wa kufanya mabadiliko makubwa katika viwanja vya ndege vya Zanzibar ikiwemo kuweka vifaa vya kisasa vya kugunduwa vitu vya hatari ikiwemo madawa ya kulevya,” alisema.
Aidha, aliitaka Wizara ya Mawasiliano na Miundombinu ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuufanyia ukarabati mkubwa Uwanja wa Ndege wa Karume uliopo Pemba ambao hadi sasa hauna taa za kuruhusu ndege kutua usiku.
Suala la Uwanja wa Ndege wa Karume ulioko Pemba kukosa huduma za taa za kuruhusu ndege kutua usiku,wajumbe wengi zaidi kutoka Pemba walitishia kuzuia bajeti hiyo.
“Mimi siungi mkono hadi pale nitakapopewa maelezo lini Uwanja wa Ndege wa Karume Pemba utawekwa taa zitakazoruhusu ndege kutua nyakati za usiku,” alisema Saleh Nassor Juma, Mwakilishi wa Jimbo la Wawi kwa tiketi ya CUF.
Uwanja wa ndege wa Karume uliopo Pemba hauna huduma za taa usiku ambapo ndege haziwezi kutua nyakati hizo na hivyo kusababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi.

No comments: