Maadhimisho ya mwaka huu ya Siku ya
Mtoto wa Afrika, yataadhimishwa nchini Jumatatu Juni 16, mwaka huu katika ngazi
ya mkoa.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia
na Watoto, Sophia Simba alisema hayo mjini hapa jana kwenye mkutano wake na
waandishi wa habari.
“Maadhimisho ya mwaka huu ya Siku ya
Mtoto wa Afrika, yataadhimishwa katika ngazi ya Mkoa, ambapo kila mkoa
utaadhimisha siku hii kwa kushirikisha halmashauri za wilaya, manispaa, miji,
kata, vijiji, mashirika na taasisi mbalimbali zilizoko katika mkoa husika na
watu binafsi,” alisema Waziri Simba.
Simba alisema hatua ya kufanya
sherehe hizo katika ngazi ya Mkoa, itaipa mikoa nafasi nzuri ya kutafakari
matatizo yanayolikabili kundi hili la watoto, ikiwa ni pamoja na kuwapatia haki
zao za msingi.
“Mikoa itapata pia nafasi ya
kufikiria kuweka miradi endelevu kwa ajili ya watoto hawa,” alisema.
Alisema maadhimisho ya kila mwaka,
huwa na kaulimbiu yake na kwamba kaulimbiu ya mwaka huu ni: “Kupata Elimu Bora
na Isiyo na Vikwazo; Ni Haki ya Kila Mtoto”.
Alisema kaulimbiu hiyo, inalenga
kukumbusha wazazi, walezi, serikali na jamii kuhusu umuhimu wa kumuendeleza
mtoto bila kumbagua, kulingana na rangi, jinsi na hali aliyokuwa nayo.
Simba alisema tarehe 16 Juni ya kila
mwaka ni kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika. Siku hiyo
huadhimishwa na nchi zote wanachama wa Umoja wa Afrika (AU), kukumbuka mauaji
ya watoto wa shule, yaliyofanyika katika kitongoji cha Soweto nchini Afrika
Kusini tarehe 16 Juni 1976.
Katika tukio hilo la kusikitisha,
inakadiriwa kuwa watoto wapatao 2,000 waliuawa kikatili na serikali ya
makaburu.
No comments:
Post a Comment