Meneja Mauzo wa Kampuni ya madini ya
Tanzanite One yenye makao yake Makuu jijini Arusha, Jacques Beytel (39) raia wa
Afrika ya Kusini amekamatwa na maofisa wa Idara ya Uhamiaji mkoani Arusha kwa
kosa la kufanya kazi nchini bila ya kuwa na kibali.
Kukamatwa kwa raia huyo wa Afrika ya
Kusini aliyekuwa akifanya kazi ya mauzo katika Ofisi Kuu za Tanzanite One
zilizopo barabara ya India jijini Arusha tangu mwaka 2008 zimethibitishwa na Ofisa
Mkuu wa Uhamiaji Mkoa wa Arusha,Daniel Namomba.
Namomba alikiri kukamatwa kwa Beytel
alipofuatwa ofisini kwake kuzungumzia tukio hilo na alisema kuwa mtuhumiwa
alikamatwa Juni 11 mwaka huu ofisini kwake bado anashikiliwa na maofisa wake
kwani mahojiano bado hayajakamilika.
‘’Tunamshikilia Beytel ambaye ni
raia wa Afrika ya Kusini kwa kosa la kufanya kazi nchini bila ya kuwa na kibali
na anahojiwa na maofisa wake,mahojiano yakikamilika itawapa taarifa na hiyo
inaweza kuwa wiki ijayo,’’ alisema Namomba
Kwa mujibu wa habari kutoka ndani ya
Kampuni ya Tanzanite One zinasema kuwa Beytel aliwahi kufukuzwa kazi mwanzoni
mwa mwaka 2008 akituhumiwa kwa wizi wa madini kurudishwa kwao kwa kosa hilo.
Habari ziliendelea kusema kuwa
haikueleweka meneja huyo alirudishwaje kazini tena kwa wadhifa huo huo, wakati
alifukuzwa kazi kwa tuhuma za wizi.
Meneja Uhusiano wa Kampuni ya
Tanzanite One ambaye pia ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo kwa sasa,
Doto Mwidadi alikiri kukamatwa kwa meneja huyo.
Mwidadi alisema vibali vya kufanya
kazi vya raia wa Afrika ya Kusini wanaofanya kazi Tanzanite One hutolewa
Uhamiaji makao makuu hivyo wamewasiliana na viongozi wa Uhamiaji makao makuu
ili waweze kuvituma Arusha.
No comments:
Post a Comment