Serikali inaandaa Muswada wa Sheria
ya Bajeti, ambao utakamilika kabla ya mwisho wa mwaka 2014/15.
Waziri wa Fedha, Saada Salum
Mkuya alisema hayo aliposoma hotuba ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka
2014/15.
“Bajeti hii imelenga pia kuimarisha
zaidi usimamizi na udhibiti wa matumizi ya fedha za umma. Ili kutekeleza azma
hii, serikali inaandaa Muswada wa Sheria ya Bajeti,” alisema.
Saada alisema Sheria hiyo inalenga
kuongeza nidhamu ya matumizi na uwajibikaji kwa wadau wote, wanaotekeleza
Bajeti ya Serikali.
Alitaja wadau hao kuwa ni viongozi
na maofisa wa serikali, wabunge, mashirika ya umma, wakala na taasisi za
serikali, makandarasi na wazabuni.
Alisema katika kuandaa muswada huo,
wadau muhimu, ikiwemo wabunge watashirikishwa kupitia kamati za kudumu za
Bunge.
Aidha, alisema katika mwaka 2014/15,
Sh bilioni 8.7 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa hospitali tisa za
mikoa nchini.
Mikoa hiyo ni Katavi, Simiyu,
Njombe, Geita, Arusha, Pwani, Kilimanjaro, Singida na Tabora.
No comments:
Post a Comment