Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni
imetoa Sh milioni 54 kwa kata zake zote 27 zilizopo katika manispaa hiyo,
kuhakikisha barabara za mitaa zinajengwa kwa kiwango cha lami nyepesi na
kifusi.
Ofisa Mahusiano wa Manispaa ya
Kinondoni, Sebastian Muhowera aliliambia gazeti hili juzi Dar es Salaam kuwa
licha ya kusubiri fedha walizoziomba kutoka serikalini kurekebisha barabara
zilizoharibiwa na mvua, kila kata inaendelea na ujenzi wa barabara hizo. Kila
kata itapata Sh milioni mbili kwa ajili ya ukarabati huo.
Alisema kazi hiyo wameziachia kila
Serikali za mitaa kwani wao wanajua barabara zao na kwamba Manispaa yenyewe
itahusika na barabara kuu na matengenezo madogo ambayo yanagharimu Sh bilioni
8.4.
Alisema kata husika zinatambua
mgawanyo wa fedha hiyo na sasa wanatoa ratiba ya maendeleo ya ujenzi katika
barabara zote zilizopo katika kata hizo.
Pia, alisema wameandaa tingatinga
ambalo litatumiwa na kata endapo watahitaji kutoka manispaa kwa ajili ya
uchongaji wa barabara na kushindilia kifusi, kwa kuwa wanataka barabara zote
ziwe na kifusi cha moramu na sio udongo.
"Katika mwaka huu wa fedha
unaoanza Julai mwaka huu, tumejipanga kuhakikisha kila barabara iliyopo katika
manispaa yetu inakuwa katika kiwango cha lami nyepesi au kifusi,’’alisema
Muhowera.
Aliongeza kuwa kiasi walichotoa kwa
kata ni kutokana na asilimia 20 ya mapato yanayokusanywa na serikali za mitaa
yanabaki katika akiba yao. Alisema mapato hayo yanatokana na leseni za sheria
za barabara.
Aidha, katika kufanikisha bajeti ya
mwaka 2014/15 Manispaa imeweka mpango wa kudumu kujenga barabara ya lami na
kituo cha daladala kuepusha wanaoegesha katika hifadhi za barabara.
Alisema ifikapo Julai mwaka huu
wataanza ujenzi wa barabara na kituo cha daladala maeneo ya Goba, Bunju,
Mabwepande na kuongeza kuwa watahakikisha barabara hizo zinatumika kwa muda
mrefu.
"Tumeunda kitengo kinachohusika
na ujenzi wa barabara ambao watasimamia na kukagua barabara zote za kata na
barabara kuu kuhakikisha kazi inafanyika kwa usahihi," aliongeza.
No comments:
Post a Comment