ASKARI WAWILI WA TPA WAPANDISHWA KIZIMBANI



Askari wawili wa Mamlaka ya Bandari Tanzania(TPA), Jonas Bakari (25) na Hashim Salum (43) wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kumkata mtu mkono.
Akisomewa mashitaka, Mwendesha Mashitaka, Vitalia Kidabulo mbele ya Hakimu Catherine Kioja alidai washitakiwa hao walitenda kosa hilo Mei 30 mwaka huu  katika geti la Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).
Alidai washitakiwa hao walimkata mkono wa kushoto Omary Hamza na kumsababishia maumivu huku wakijua kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Washitakiwa  wote wako nje kwa dhamana iliyowataka kuwa na wadhamini wawili kila mmoja na kiasi cha Sh milioni moja  kila mmoja na kesi itatajwa tena Juni 30 mwaka huu. 
Katika tukio jingine, mkazi wa Chanika, Shukuru Bakari (25) amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya Ilala kwa tuhuma za kulawiti mtoto wa miaka 11.
Akisomewa mashitaka yake na Mwendesha Mashitaka  Anunciath Leopold mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi,  Hassan Juma, alidai mshitakiwa huyo alitenda kosa hilo Septemba mwaka 2013 huko Chanika Wilaya ya Ilala.
Alidai mshitakiwa huyo alimlawiti mtoto wa miaka 11 huku akijua kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Mshitakiwa alikana mashitaka yake na amerudishwa rumande mpaka Juni 26 mwaka huu kesi itakapotajwa tena.

No comments: