Serikali itaanzisha mfumo mpya wa
kielektroniki wa kununua, kutunza na kuuza mafuta yanayotumika katika magari
yake.
Hayo yalibainishwa na Waziri wa
Fedha, Saada Salum Mkuya aliposoma Hotuba ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka
2014/15.
Alieleza kuwa ili kudhibiti matumizi
na kupata thamani ya fedha katika ununuzi wa bidhaa na huduma, serikali
imeamua kuzingatia ununuzi wa pamoja (bulk procurement) kutoka kwa wazalishaji
badala ya wakala, kama ilivyo sasa; na hatua imeanza kuchukuliwa ili ununuzi wa
magari na vyombo vya TEHAMA ufuate utaratibu huo.
“Aidha, kutokana na wingi wa mafuta
yanayotumika kwenye magari na mitambo, serikali itaanzisha mfumo mpya wa
kielektroniki, utakaotumika katika kununua, kutunza na kuuza bidhaa hiyo ili
kuwezesha serikali kupata thamani halisi ya fedha zinazotumika katika ununuzi
wa mafuta,” alisema.
Vilevile, Waziri huyo wa Fedha
aliagiza vitabu vya kumbukumbu (diaries) na kalenda za kila mwaka, kuanzia
mwaka 2014/15 zitachapishwa na Ofisi ya Waziri Mkuu tu.
“Hii ni kwa wizara, idara
zinazojitegemea, wakala na taasisi za serikali, mikoa na mamlaka za serikali za
mitaa, badala ya utaratibu wa sasa ambapo kila taasisi ya serikali inachapisha
kwa utaratibu wake” alisema.
Pia,
alisema ili kupunguza matumizi ya umeme katika ofisi za serikali, serikali
inatarajia kutumia vifaa vya umeme vyenye matumizi kidogo ya umeme (energy
saving technology sensors).
No comments:
Post a Comment