WALIOZAA WAKIWA SHULENI KUSAKWA WARUDI DARASANI



Wilaya  ya Mpanda  mkoani Katavi  itafanya operesheni maalumu  ya kuwasaka, kuwakamata  na kuwarejesha  shuleni  wanafunzi  wote  waliokatiza  masomo kwa utoro  na ambao tayari wameshazaa.
Mkuu  wa Wilaya ya Mpanda, Paza Mwamlima alibainisha hayo  wakati  wa kikao cha Kamati ya Maendeleo ya Kata kilichofanyika jana  na kubainisha kuwa atalitumia  jeshi  la Polisi  kuendesha  msako  huo unaotarajia kuanza rasmi  Julai  mwaka huu.
Pia  amewaagiza  wazazi  na walezi  wa  wanafunzi  waliokuwa  wakisoma katika Shule  ya Sekondari  Mpandandogo, Tarafa ya Kabungu  wilayani  hapa  ambao  wakatiza masomo  yao  baada ya kuoa na kuolewa wahakikishe  wanawarejesha  shuleni  na kuanza masomo  mara moja .
“Wazazi  na walezi  hakikisheni watoto  wenu  waliokatiza  masomo  kwa  utoro, kuolewa  au  kuoa  pia  hata wale  waliokwishazaa  mnawarejesha  shuleni  kuanza masomo  mara moja  atakayekaidi  agizo  hili  atachukuliwa  hatua kali  zikiwemo za kisheria...kwani  sasa  hatuwezi tena  kufumbia  macho  jambo  hili," alisisitiza.
Mkutano  huo wa Kamati ya Maendeleo  ya kata  uliofanyika  katika  Shule ya Sekondari  Mpandandogo katika Kata ya Kabungu ilijumuisha  wazazi, walezi  na wanafunzi  ili  kujadili  kwa kina  maendeleo  ya elimu ya shule hiyo  ambayo ilishika nafasi  ya  mwisho  kwa ufaulu  wa wanafunzi  katika Mtihani  wa Taifa wa kuhitimu Kidato  cha Nne  mwaka jana  kwa  shule  zote za sekondari mkoani  Katavi.
Aliongeza kuwa amelazimika kutoa maagizo  hayo  kutokana na taarifa  kwamba shule ya Sekondari Mpandandogo  imekuwa ikifanya  vibaya katika  mitihani  ya kitaifa  kutokana na  sababu mbalimbali zikiwemo utoro uliokithiri.
Sababu zingine zilitajwa kuwa  wanafunzi kukatiza masomo  ambapo wazazi wao wenyewe  wanawaoza watoto wao  wa kiume  na kuwaozesha mabinti zao  likichukuliwa kuwa ni jambo  la kawaida kabisa.
Awali Mkuu wa Shule ya Sekondari Mpanda ndogo, Rashid  Msyete alieleza kuwa shule hiyo yenye kidato cha kwanza hadi  cha nne  ina  idadi  ya wanafunzi  165  kati yao  wanaume ni 104  na wasichana  61  wakati  shule hiyo ina  nafasi  ya kusomesha  wanafunzi 600 kwa wakati  mmoja.
Naye mzazi Veronica Godfrey,  alieleza kuwa wanafunzi wengi wa shule hiyo wamekuwa ni watoro kutokana na adhabu  kali zinazotolewa na walimu shuleni hapo pindi mwanafunzi anapokuwa amefanya kosa hata likiwa ni kosa dogo la kinidhamu.
“Hii adhabu  inayotolewa na  walimu  wanapowaadhibu  wanafunzi  maarufu  kama “kunyonya  mafuta” ni kikwazo  kikubwa sana  kwa wanafunzi  ambapo  imesababisha wengi  wao   kuwa watoro,”  alisema  Veronika. 
Ndipo Mkuu wa Wilaya, Mwamlima  aliposimama na kuagiza  wanafunzi  wa shule hiyo  watoe  ufafanuzi  wa  adhabu hiyo  ndipo  alipoelezwa  kuwa  adhabu  hiyo ya kunyonya mafuta   kwamba mwanafunzi  anapoadhibiwa  analazimishwa  aweke  kichwa chake  chini  ardhini  huku  miguu  yake  ikiwa  juu  hewani.

No comments: