DK BILAL ACHANGIA SHILINGI MILIONI 10 MFUKO WA ELIMU KIBAHA

Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal ameuchangia Mfuko wa Elimu wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha mkoani Pwani kiasi cha Sh milioni 10. Akizungumza wakati wa kuchangia fedha  mfuko huo,  Dk Bilal alisema katika kufikia malengo ya Matokeo Makubwa Sasa (BRN) kwenye sekta ya elimu lazima kuwe na mikakati maalumu ya kuweza kufikia malengo kwa kukabiliana na changamoto zilizopo kwenye sekta hiyo. 
“Nawapongeza kwa kuanzisha mfuko huu na serikali itawaunga mkono kwa hali na mali na mimi nawachangia Sh milioni 10 kwa ajili ya kukabiliana na changamoto kwenye sekta ya elimu katika mji wa Kibaha, wilaya na mkoa mzima wa Pwani," alisema. 
Fedha hizo za mfuko wa elimu zitatumika kujenga maabara tatu katika sekondari za Pangani, Visiga na Miembe Saba na kununua madawati 1,500 kwa ajili ya shule za msingi za Tandau, Lulanzi, Misugusugu, Zogowale, Msangani, Viziwaziwa, Vikawe, Mwanalugali, Mkuza na Kidimu. 
Awali Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Kassim Majaliwa ambaye wizara yake ilichangia Sh milioni tano, alisema ubunifu wa kupata fedha kwa ajili ya Halmashauri 167 hapa nchini ni mzuri, kwani utasaidia kukabiliana na changamoto zilizopo kwenye sekta ya elimu. 
Kwa upande wake mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini, Silvestry Koka aliyechangia Sh milioni 16, alisema kuwa amefurahishwa na uzinduzi huo ambapo alisema moja ya ndoto zake ni kukabiliana na changamoto za elimu. 
Mwenyekiti wa mfuko huo, Anna Bayi alisema kuwa lengo la kuanzishwa mfuko huo ni kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia ambapo hadi sasa mfuko huo una kiasi cha sh milioni 210 na ahadi ni Sh milioni 34 huku malengo yakiwa ni kukusanya kiasi cha sh milioni 300.

No comments: