RASIMU MISWADA YA SHERIA YA USALAMA WA MITANDAO YAKAMILIKA



Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia imekamilisha rasimu ya miswada mitatu ya sheria za usalama wa mtandao ili kudhibiti uhalifu katika mitandao.
Akiwasilisha makadirio ya bajeti ya wizara hiyo, Waziri Profesa Makame Mbarawa alitaja miswada hiyo kuwa ni Sheria ya Usalama wa Mtandao, Sheria ya kulinda Taarifa Binafsi, Sheria Miamala ya Kielektroniki na sheria ya Kudhibiti Uhalifu wa Mtandao na Kompyuta.
Alisema rasimu hizo zimewasilishwa kwa mwanasheria Mkuu wa Serikali ili ziweze kuandaliwa kwa mujibu wa taratibu za uandishi wa sharia.
Pia alisema  wizara hiyo imetengeneza kanuni mpya zinazosimamia mawasiliano kupitia mitandao ya simu ambao ulianza kazi mwezi Oktoba mwaka jana kwa kampuni za nje kutakiwa kulipa senti 25 za Marekani kwa kila dakika moja ya mazungumzo ya simu zinazoingia nchini  kutoka nje.
Alisema katika kanuni hiyo mpya, imeweka mgawanyo wa mapato hayo ya senti 25 ambapo serikali kupitia hazina inapata senti saba, watoa huduma wanapata senti 13 na senti tano ni kwa ajili ya uendeshaji wa mitambo ikiwa ni pamoja na kumlipa mwekezaji wa mitambo huo.
“Hadi kufikia mwezi Januari mwaka huu, mfumo huu umeweza kuingizia Serikali jumla ya shilingi bilioni 6.8, mtambo huo pia unaratibu dakika za maongezi kwa simu za kimataifa na kufuatilia udanganyifu kwa simu zinazoingia nchini ambapo mpaka sasa udanganyifu umepungua kutoka asilimia 60 kabla ya mdandao huo kufungwa hadi asilimia mbili,” alisema.
Alisema katika kuweka mazingira mazuri ya kukuza sekta ya mawasiliano na kuimarisha uratibu pia wizara imekamilisha uandaaji wa rasimu ya sera mpya iliyohuishwa na rasimu ya mkakati wa utekelezaji wa sera mpya.
Akiwasilisha maoni ya kamati ya Miundombinu, Makamu Mwenyekiti Juma Kapuya alishauri Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuongeza nguvu katika kusimamia usalama wa mawasiliano ya mtandao wa kompyuta kwa hali ilivyo sasa kumekithiri wizi na utapeli katika mitandao.

No comments: