MABOHORA KUPANDA MITI KESHO



Jumuiya  ya Mabohora  nchini  Tanzania   inatarajiwa kupanda miti kesho jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia shughuli hiyo, Seifeddin Jamali ambaye ni mmoja wa watendaji wa  jumuiya hiyo, alisema shughuli hiyo itawakilisha  siku ya upandaji miti duniani inayoratibiwa na Jumuiya ya Mabohora ulimwenguni kote.
Alisema, jumuiya hiyo huadhimisha  siku  ya upandaji miti kila ifikapo Juni 2 ya kila mwaka kote waliko wanajumuiya ikiwemo Tanzania.
Alisema kwa mwaka huu watashirikiana na Manispaa ya Ilala kwa ajili ya kulifanya  jiji la Dar es Salaam kuwa la kijani.
Alisema, eneo litakalohusika ni la Uwanja wa Ndege jirani na kiwanda cha  Bakhressa ambapo jumla  ya miche 1,252 itapandwa.
Alisema, miche  hiyo ni ya aina  mbalimbali ikiwemo jamii ya mitende na itapandwa katika maeneo mengi ya wazi  ikiwemo kando kando  na eneo la katikati la Barabara ya Nyerere.
Aliongeza kuwa, pamoja na watu mbalimbali, shughuli hiyo itahudhuriwa pia na Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa na baadhi ya watendaji wake.
Alitoa mwito kwa wakazi wa maeneo jirani  kuungana na wanajumuiya na Manispaa ya Ilala katika zoezi hilo la upandaji miti likaloanza saa tatu asubuhi.

No comments: