WAHISANI WAANZA KUTEKELEZA AHADI BAJETI YA 2013/2014


Kilio cha wabunge kuhusu baadhi ya wizara kukosa fedha kama zilivyoidhinishwa na Bunge katika Bajeti inayoisha,  kimesikika ambapo mazungumzo kati ya Serikali na wahisani, yamezaa matunda kwa baadhi ya wahisani kukubali kutoa fedha hizo kabla la Juni 30, mwaka huu.
Akitoa majumuisho ya michango mbalimbali ya wabunge, waliojadili hotuba ya makadirio ya bajeti ya Wizara ya Fedha juzi, Waziri wa Fedha, Saada Salum Mkuya, alisema tayari washirika kadhaa wa maendeleo, wameshaiarifu Wizara kwamba watatoa fedha zao kabla ya tarehe hiyo, ambayo ndiyo mwisho wa mwaka wa fedha unaoisha.    
“Kwa mfano, Japan imesema tutasaini mkataba wa kutoa fedha hizo tarehe 16 Juni,” alisema Saada. 
Katika mkutano wa Bunge la Bajeti unaoendelea, wizara nyingi zililalamikiwa kwa kutotekeleza Bajeti inayoisha, hasa Wizara ya Maji ambayo mpaka wakati hotuba ya makadirio ya bajeti yake ya mwaka ujao wa fedha ikisomwa, ilikuwa imepelekewa fedha kidogo. 
Mpaka wakati makadirio ya bajeti ya Wizara ya Maji kwa mwaka 2014/2015 yakisomwa bungeni Jumamosi iliyopita, Serikali ilikuwa haijaipatia Wizara hiyo kwa wakati Sh bilioni 138.3, zilizoidhinishwa na Bunge kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji vijijini kwa mwaka wa fedha wa 2013/14.
Taarifa za fedha zilionesha kuwa hadi kufikia Aprili mwaka huu, Serikali ilikuwa imeipatia Wizara ya Maji Sh bilioni 39.4 tu, kati ya Sh bilioni 138.3 zilizoidhinishwa sawa na asilimia 28 ikiwa ni pungufu ya Sh bilioni 98.9.
Kutokana na hali hiyo, Kamati ya Bunge ya Bajeti chini ya Mwenyekiti wake, Andrew Chenge, awali iliizuia wizara hiyo kuwasilisha bungeni makadirio ya bajeti yake ya 2014/15 na kuiagiza Serikali kuipatia wizara hiyo kiasi hicho cha fedha mapema iwezekanavyo.
Kamati ya Bunge ilichukua hatua hiyo ikiamini kwamba wabunge wangezuia makadirio ya bajeti ya Wizara ya Maji, kutokana na kutopewa kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji vijijini.
Katika hotuba yake bungeni, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge, Kilimo, Mifugo na Maji, Profesa Peter Msolla, alisema Serikali ilipaswa kuipatia wizara kiasi hicho cha fedha kilichosalia kabla ya  Mei 31, mwaka huu, ambayo ni siku aliyokuwa imepangwa awali kabla ya kuahirishwa, kwa ajili ya kusomwa kwa makadirio ya bajeti ya Wizara ya Maji.

Kutokana na hali hiyo, Spika wa Bunge, Anne Makinda, alimrushia suala hilo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ili atoe majibu ya Serikali katika suala hilo.
Pinda alisimama na kueleza kuwa aliiona hotuba ya kamati hiyo na kwamba Serikali ilipanga kuipatia wizara hiyo Sh bilioni 80 kabla ya mwisho wa Mei, mwaka huu.
“Hadi Juni, mwaka huu, tunatarajia tutakuwa tumepata kiasi kingine...itabidi tunyofoe hata kutoka kwenye posho mbalimbali na kama tutashindwa, basi wabunge itabidi mtuelewe tu,” alisema Pinda kwa utulivu.
Mbali na Japan kueleza kuwa itakamilisha ahadi zake Juni 16,  Waziri wa Fedha, Saada alisema Serikali imeanza kikao cha siku mbili na washirika wa maendeleo mjini Dodoma kuanzia jana, ili watimize ahadi zao zilizochangia baadhi ya wizara kupewa mafungu pungufu ya fedha zilizoidhinishiwa na Bunge katika bajeti inayoisha.

Alisema lengo la kikao hicho ni kujadiliana na washirika hao, waeleze utekelezaji wao wa kutoa fedha walizoahidi, kuchangia Bajeti Kuu ya Serikali.
“Tutakuwa na mkutano na washirika wa maendeleo hapa Dodoma kwa siku mbili kuanzia kesho (jana), tutajadiliana nao na kuwaomba wakamilishe  ahadi  zao kabla ya tarehe 30 Juni mwaka huu,” alisema Saada.
Waziri wa Fedha alisema mbali na kufanya vikao na washirika wa maendeleo, Wizara yake inaendelea kutafuta fedha kutoka katika vyanzo mbalimbali ili kuzipeleka katika wizara, ambazo mafungu ya bajeti  zake, hayajakamilika.
Saada alitaja baadhi ya wizara ambazo zimepata mafungu kidogo hadi sasa, hivyo zinahitaji kupelekewa kiasi kilichobakia kuwa ni pamoja na Wizara ya Maji na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii. 
Waziri huyo pia alisisitiza umuhimu kwa Watanzania kulipa kodi,  kwa sababu Serikali inapata fedha zake kupitia kodi mbalimbali. Alisema kila mtu ana wajibu wa kulipa kodi na kudai risiti.
Alisema mtu asiyelipa kodi, anainyima Serikali mapato yake na ni chanzo kimojawapo cha Serikali kushindwa au kuchelewa kupeleka mafungu kwa wizara nyingine.

No comments: