BAJETI KUU YA SERIKALI YASUKWA



Kamati ya Bajeti  ya Bunge la Jamhuri ya Muungano, jana ilianza vikao vya siku sita na Serikali ili kutayarisha Bajeti Kuu ya Serikali, ambayo itasomwa Juni 12, mwaka huu na Waziri wa Fedha, Saada Salum Mkuya.
Hatua hiyo ni ya mara ya pili kwa Serikali na Bunge kukaa pamoja kutengeneza Bajeti Kuu ya Serikali, ambapo mara ya kwanza ilianza katika Bunge la Bajeti la mwaka jana.
Hali hiyo ni tofauti na miaka iliyopita, ambapo Bajeti Kuu ya Serikali, ilikuwa inatayarishwa na Serikali  peke yake.
Taarifa hiyo ilitolewa bungeni mjini hapa jana na Spika wa Bunge, Anne Makinda alipokuwa akielezea ratiba ya shughuli za Bunge hadi sasa.
“Zile siku 26 za kujadili wizara zimekwisha jana. Katika siku zote hizo tulikuwa tunajadili sekta moja moja, lakini leo (jana) hadi
tarehe 11 Juni  Kamati ya Bunge itajadiliana na Serikali kwa undani zaidi juu ya utekelezaji wa bajeti ya sasa na utayarishaji wa bajeti kuu ijayo.
Kipindi hiki Bunge linashiriki katika kutengeneza Bajeti ya Serikali,” alisema Spika.
Alieleza kuwa majadiliano hayo, baina ya Serikali na Kamati
ya Bajeti, yatahusisha pia wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge.
Spika alitaja wizara ambazo Wizara ya Fedha, itajaribu  kutafuta fedha katika vyanzo vyake mbalimbali kukamilisha bajeti za wizara hizo.
Kuwa ni Wizara ya Maji, Wizara ya Nishati na Madini na Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia.

No comments: