WAHASIBU, WAKAGUZI WA MADENI FEKI KUTIMULIWA KAZI

Muswada wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2014 umepita jana huku Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, akitoa onyo kwa wahasibu watakaopeleka madai ya madeni yaliyochakachuliwa kuwa atawafukuza kazi.
Akichangia hoja jana, Nchemba alisisitiza kuwa Serikali italipa madeni yote lakini baada ya kufanya uhakiki na wakigundua kuwa yaliongezwa, mhasibu na mkaguzi wa mahesabu waliopitisha madai hayo, watafute kazi zingine.
“Hapa kwa kweli tuko tayari kuondoa timu nzima ofisini na kuweka mpya…wako vijana wana shida ya kazi hawajaanza kupasha bora tuwape wao na kama kuna shida ya kisheria, Mama Kombani (Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Utumishi, Celina), lete sheria  ili fedha za Serikali ziheshimiwe,” alisema.
Alikumbushia mfano uliotolewa na Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum, kuwa katika uhakiki walibaini madeni feki yaliyoletwa Hazina kwa ajili ya malipo.
Katika mfano huo alisema kuna deni lilipelekwa Hazina la Sh milioni 600 kwa ajili ya malipo lakini uhakiki ulipofanyika, deni halisi lilibainika ni Sh laki sita tu. Mfano mwingine ni wa deli la Sh trilioni 1.5 na uhakiki ulipofanyika ikakutwa deni halisi ni la Sh milioni 150.
Naye Naibu Waziri wa Fedha, Adam Malima, akizungumzia nidhamu ya fedha za Serikali, alitolea mfano wa Kodi ya Majengo, ambapo alisema nyumba 50 za Dar es Salaam katika mitaa kama ya Oysterbay, Masaki, Msasani na Mikocheni, zinaweza kulipa kodi hiyo katika mji mzima kama wa Mbeya.
“Sasa hizi hazikusanywi, idara za ardhi katika halmashauri kama zimeshindwa kazi hapa ndipo Mwigulu anasema, watoke waingie wengine wafanye kazi,” alisema Malima.
Nchemba pia alitetea uamuzi wa Serikali kwa mashirika yote ya umma na tasisi zinazokusanya maduhuli wapeleke bajeti zao kwa Mlipaji Mkuu wa Serikali ili zidhibitiwe.
“Hivi mnajua leo hii kuna timu nzima ya Shirika inasafiri kwenda nje kufanya semina na wote wanapanda ndege daraja la kwanza na la pili…tunataka semina hizo Mlipaji Mkuu wa Serikali azizuie,” alisema Nchemba.
Pia aliagiza taasisi hizo kuanza kukusanya maduhuli  kwa kutumia mfumo wa kielektroniki, ili kila wanachokusanya  kionekane huku akisisitiza kuwa haiwezekani  Serikali inawataka wafanyabiashara wadogo kutumia mashine za kodi za kielektroniki (EFDs), wakati taasisi za Serikali zinatoa na kutumia risiti za kuandika kwa mkono. 
Kuhusu misamaha ya kodi, Nchemba alimpongeza Waziri wa Fedha Saada kwa kujiondolea madaraka ya kusamehe kodi na kusema huo ni ujasiri mkubwa.
Alisema hata kwa misamaha ambayo imeshatolewa, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), atakwenda kuikagua ili kubaini kama ilitumika kama ilivyokusudiwa.
“Silaha ya fedha ya kupunguza pengo la walionacha na wasionacho ni kutoza kodi kwa matajiri na kumpa huduma masikini…ukimtoza masikini na kumsamehe tajiri, masikini ataendelea kuwa masikini na tajiri ataendelea kuwa tajiri,” alisema Nchemba.
Naye Waziri Mkuya katoka suala la misamaha ya kodi, alisema pamoja na Muswada wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na Muswada wa Menejimenti ya Kodi kusogezwa mbele, Serikali itairejeshwa tena Bunge la Novemba.
“Katika misamaha ya kodi ya mafuta, hakuna siku hata moja faili la misamaha ya kodi linakaa mezani kwangu kwa siku mbili, inauma na inasikitisha sana, tunawapa ruzuku hawa wawekezaji wakati wanapata faida,” alisema Saada.
Nchemba katika hilo, alisema aliwahi kuzungumza na mwekezaji mmoja kuhusu msamaha wa kodi, akamuuliza ni wapi kwingine duniani kitu hicho kinafanyika, akamjibu hakuna lakini kwa kuwa Tanzania tuliweka katika sheria kuwa wanastahili msamaha, ndio maana wanafuatilia stahili yao hata kama wanapata faida.
Kuhusu Ushuru wa Ujuzi na Maendeleo (SDL) ambao unakwenda katika Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, ambayo baadhi ya wabunge walipendekeza ipunguzwe, Nchemba alisema haitapunguzwa.
“Hiki ndio chanzo muhimu cha fedha za Bodi mnataka kipunguzwe wakati mwaka jana zaidi ya wanafunzi 12,000 walikosa mkopo?
“Mtoto anasomeshwa kwa vitumbua mpaka anafika kidato cha sita na mimi ningependa kila anayekubalika kujiunga na chuo apate mkopo, si fedha za bure ni mkopo ambao akimaliza shule analipa, hapa wanakosa si haki,” alisema huku akitetea kuwa kodi hiyo isipunguzwe.

No comments: