WAFANYABIASHARA WALIOPOTEZA MALI MCHIKICHINI WAORODHESHWA



Wiki moja baada ya moto kuteketeza soko la Mchikichini, wafanyabiashara wa soko hilo waliopoteza mali zao wameorodheshwa majina yao ili kusaidiwa ikiwemo orodha hiyo kupelekwa kwenye taasisi za fedha kuomba wafanyabiashara hao waongezewe muda wa makato ya mikopo waliochukua.
Akizungumza na mwandishi jana, Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Mitumba sokoni hapo, Hajali Mohamed alisema kuwa moto huo umeteketeza mali za wauza  mitumba 3,800.
Alisema kutokana na hali hiyo, uongozi wa soko hilo ukishirikiana na Serikali ya Mtaa Mchikichini umeanzisha utaratibu wa kuandika barua zinazowatambulisha wafanyabiashara waliopoteza mali zao ambazo zinapelekwa kwenye taasisi mbalimbali za fedha walizokopa.
Alisema kuwa moto umeathiri mitaji ya wafanyabiashara mbalimbali na ambao hawana uwezo wa kurejesha mikopo kwa wakati kama wanavyotakiwa na taasisi husika za fedha walizokopa, hivyo barua hizo maalumu walizopewa zinawatambulisha kwenye taasisi hizo kuwa ni waathirika wa moto huo.
"Uandikishaji huu umeanza leo (jana) na kesho (leo) suala hili litamalizika na kisha kujua ni wafanyabiashara wangapi wamepewa barua za kuwatambulisha kwenye taasisi za fedha kwa ajili ya kusaidiwa kwenye urejeshwaji wa mikopo," alisema Mohamed.
Aliongeza kuwa pia Kamati ya Maafa ya Mkoa imewataka wafanyabiashara hao kuorodhesha mali za wafanyabiashara hao zilizopotea ifikapo kesho.
"Naipongeza kamati hiyo kwa hatua ambayo inaonekana kuwa ni nzuri na itakuja kuwa yenye mafaniko pengine kwa baadaye manake mali zilizoteketea hapa ni nyingi na sijui kama itawezekana kwa kila mfanyabiashara kujigharimia mwenyewe katika kuimarisha mtaji wake," alisema Mohamed.
Mwandishi alifanya ufuatiliaji wa hali inavyoendelea sasa sokoni hapo  na kuona wafanyabiashara mbalimbali wakijengea mabanda yao huku wengine wakiwa wameanza kufanya biashara zao kama kawaida.
Sehemu kubwa ya maeneo yaliyokuwa yameungua yameanza kujengwa upya ambapo wajenzi wamekutwa wakijenga mabanda na kuweka mabati.

No comments: