Chama cha Uzazi na Malezi Bora Tanzania
(UMATI) kimekabidhi baiskeli 40 zenye thamani ya sh milioni 4.8 wahudumu
wa afya ya uzazi na ujinsia ngazi ya jamii waliopo katika Kata za Chumbi 'A' na
Bungu zilizopo wilayani Rufiji, Mkoa wa Pwani.
Akizungumza wilayani hapa mwishoni mwa
wiki, Mkurugenzi Mtendaji wa UMATI, Lulu Ng'wanakilala katika hotuba yake
iliyosomwa na Meneja Miradi wa UMATI, Tausi Hassan alisema lengo la kukabidhi
baiskeli hizo ni kuunga mkono juhudi za Serikali za kuboresha afya ya mama na
mtoto .
Ng'wanakilala alisema UMATI kupitia
ufadhili washirika la MERCK Sharp and Dohme (MSD) kutoka nchini Marekani
liliweza kupata mradi wa uwiano katika ubunifu wa kuboresha Afya ya Mama na
Mtoto, mradi unaotekelezwa katika kwa kipindi cha miaka mitatu katika mikoa ya
Pwani na Katavi na kushirikiana kwa karibu zaidi na Ofisi za Mganga Mkuu wa
Wilaya.
Kwa upande wake Kaimu Mganga Mkuu wa
Wilaya ya Rufiji, Rasmo Msabaha alisema Mkoa huo umepanga kufikia asilimia 60
ya malengo iliyojiwekea katika kuzuia vifo vya Mama na Mtoto na hadi kufikia
sasa umefikia asilimia 37, na hivyo jitihada za pamoja hazina budi kufanywa
katika kufikia kiasi kilichobaki.
"Uzazi wa Mpango ni muhimu sana,
hapo zamani Serikali iliweza kutoa bure huduma za afya na elimu, lakini kwa
sasa idadi ya wananchi imekuwa kubwa na ndio maana Serikali imeamua
kushirikiana na sekta binafsi ikiwemo UMATI ilikuweza kusaidia huduma za afya,
hivyo ni lazima tuzae kwa mpangilio na kwa kadri tunavyoweza kuwahudumia"
alisema.
Naye Diwani wa Kata ya Bungu, Ramadhani
Mkwaya alisema Ofisi yake imeupokea kwa moyo mmoja mradi huo na ipo tayari
kuutekeleza, na akaishukuru UMATI kuichagua Kata yake kati ya Kata 27
zilizopokatika Wilaya hiyo na kusema kuwa hicho nikielelezo kuwa Kata hiyo
inakubalika kimaendeleo.
Aidha Diwani wa Kata ya Chumbi,
Ramadhani Mikole aliwataka wahudumu hao wa afya ya uzazi ngazi ya jamii
kutokuwa kimya iwapo kutatokea tatizo la kiutendaji katika majukumu yao,na badala
yake wawasiliane mara moja na wahusika wa mradi ili kuhakikisha kuwa mradi
unafikia malengo yake.
No comments:
Post a Comment