DC APONGEZWA KUPIGA MARUFUKU STAILI YA 'KATA K'



Mkuu wa Wilaya  ya Sumbawanga, Mathew Sedoyeka amepongezwa na vijana wilayani  humo  kwa uamuzi  wake  wa  kuwapiga  marufuku  vijana  wote  wa kiume  popote wilayani  humo  kuvaa  suruali kwa mtindo wa mlegezo maarufu kama Kata K .
Hata hivyo  wamemtaka  DC huyo  apige  marufuku  wasichana  kuvaa  mavazi  yasiyo  ya  staha  ikiwemo  vipedo  na  sketi  fupi  huku  baadhi yao  wakiwa  nusu  uchi  kwamba  uvaaji  huo  nao pia hauendani   na  maadili  ya Watanzania.
Wakizungumza kwa  nyakati tofauti na mwandishi  wa habari  hizi baadhi ya  vijana  wa  kike na  kiume  wamemtaka Mkuu  huyo wa Wilaya,  kuamuru  kuwa  kijana  yeyote  akikamatwa  amevaa  mavazi  hayo  yasiyo na stahi  awe  wa kike  au  wa kiume  atozwe  faini ya  kiasi  cha Sh 50,000 na fedha  hiyo apewe  mtu aliyemkamata na kufikishwa Kituo  cha Polisi.
"Kwa  staili hii ya kupigwa faini  itatuogopesha  na  nikuhakikishie  tutaacha  tabia  hii  ya kuvaa kiajabu ajabu,"  alisema Tofilo Mbalamwezi, mkazi  wa eneo  la Majengo.
Kauli  na pongezi  hizo za vijana hao  zimekuja  siku  chache  baada ya DC kupiga  marufuku uvaaji wa suruali  kwa staili  ya Kata K  kwa kijana yeyote wa kiume mahali popote wilayani humo.
Pia Sedoyeka aliwaagiza viongozi wa serikali za mitaa, vijiji, kata tarafa na wilaya kushirikiana na Kamati za Ulinzi na Usalama katika maeneo yao ya kiutawala kuwachukulia hatua kali vijana wote wa kiume watakaobainika kuvaa suruali zao kwa staili hiyo ya Kata K.
Alitoa maagizo hayo hivi karibuni akihutubia mikutano mbalimbali ya hadhara wilayani humo ambapo  alisema tabia hiyo ya vijana wa kiume kuvaa suruali zao kinyume cha utaratibu haiwezi kuvumilika kwa kuwa inatukanisha jamii.

No comments: