SIKIKA YATAKA WABUNGE WAPIGIE DEBE BAJETI YA AFYA



Asasi ya kiraia ya SIKIKA imewataka wabunge kuishawishi Serikali kuongeza bajeti ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, kwa lengo la kukabiliana na tatizo la ukosefu wa dawa muhimu na vifaa tiba katika vituo mbalimbali vya afya nchini.
Akizungumza na waandishi mbalimbali wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Sikika Irene Kiria, alisema hatua hiyo itasaidia kutatua tatizo hilo la dawa kwani wabunge walio wengi wanalalamikia tatizo hilo.
Ombi la Sikika kwa wabunge hao limetolewa wakati Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ikitarajia  kuwasilisha makadirio ya mapato na matumizi yake  wiki hii huku kilio kikubwa cha asasi hiyo, kikilenga kuhamasisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi.
Alisema tathmini mbalimbali zinaonesha kuwa, upatikanaji wa dawa muhimu  na vifaa tiba katika vituo vya huduma za afya za umma ni mdogo; hivyo kusababisha wananchi wengi kulazimika kutafuta dawa hizo kutoka katika maduka ya kawaida.
"Kwa mfano utafiti uliofanywa na Sikika mwaka 2012 umeonesha kuwa asilimia 52 ya hospitali hazikuwa na dawa muhimu na vifaa tiba kwa zaidi ya wiki nne na moja ya sababu kuu za kukosekana kwa dawa muhimu na vifaa tiba ni bajeti ndogo inayotengwa na Serikali," alisema Kiria.
Alisema ingawa mojawapo ya vipaumbele vya Wizara ya afya ni kuboresha upatikanaji wa  dawa muhimu, mgao wa fedha kwa ajili ya ununuzi wa dawa muhimu na vifaa tiba umekuwa hauendani mahitaji yake na hivyo kutosaidia tatizo linalojitokeza.
"Kwa mujibu wa makadirio ya Wizara ya afya zinahitajika kiasi cha Sh bilioni 250 kukidhi mahitaji ya dawa muhimu kwa mwaka 2014/2015, hata hivyo mgao unaotarajiwa kupangwa ni Sh bilioni 45 sawa na asilimia 7.7 ya mahitaji yote," aliongeza Kiria.
Pia alisema pamoja na kipaumbele cha Wizara hiyo kupunguza vifo vya akinamama na watoto vitokanavyo na kujifungua, bajeti ya vifaa vya kujifungulia inapungua mwaka hadi mwaka na hivyo kuondoa matumaini ya kupunguza vifo hivyo kwa wananchi.

No comments: