TBC YAPOKEA GARI LA KISASA LA KURUSHIA MATANGAZO KUTOKA CHINA

Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) limepokea gari la kisasa la matangazo (OB-Van) lenye thamani ya Sh bilioni sita kutoka kwa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China.
Msaada huo ulikabidhiwa jana kwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk Fenella Mukangara mbele ya Makamu wa Rais wa China, Li Yiuanchhao aliyeondoka nchini jana baada ya kukamilisha ziara yake ya wiki moja nchini.
Akizungumza mara baada ya kupokea na kukabidhi funguo za gari hilo, kutoka kwa Waziri wa Biashara wa China, Li Jinzao, Dk Mukangara, alisema gari hilo litasaidia kuiongezea uwezo TBC, kama televisheni ya taifa kuzungumzia nchi zote yaani Tanzania na China kwa malengo chanya ikiwa ni pamoja na habari nyingine za ndani na nje ya nchi.
“Hii OB Van itasaidia sana katika kuiwezesha TBC kutekeleza majukumu yake kitaifa na kimataifa kama chombo cha Serikali chenye jukumu la kuwaunganisha watanzania na wananchi wengine kutoka mataifa rafiki duniani ikiwemo China,” alisema.
Alisema Tanzania ni nchi kubwa hivyo ili chombo hicho kiweze kuwafikia wananchi kwa wakati, TBC bado inahitaji gari moja kubwa kama hilo na mengine matatu madogo.
Na hiyo ni kutokana na agizo la Taasisi ya Kimataifa ya Mawasiliano(ITU) la kuzima mitambo ya analojia ifikapo Juni 17 mwakani.
Mukangara alisema kwa sasa Serikali imeanza kushughulikia suala la kuiwezesha TBC kuwa na uwezo wa dhati wa kuwafikia wananchi katika kona zote za Tanzania kwa kushirikiana na kampuni ya China ya Startimes.
Hata hivyo, alisema Oktoba mwaka huu, Rais Jakaya Kikwete anatarajiwa kufanya ziara China, ambapo akiwa na Rais Xi Jinping watazungumzia uwezekano wa Tanzania kupatiwa mkopo nafuu kwa ajili ya kuliboresha zaidi shirika hilo.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Clement Mshana, alisema gari hilo lina kamera sita za kisasa ambazo moja kati ya hizo, iko katika nchi ya Zimbabwe pekee na ilitumika kunyaka matukio muhimu katika maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano ya mwaka huu.
“Katika maadhimisho yale tulinyaka picha ambazo kamera za kawaida haziwezi ikiwemo askari walioruka kwenye ndege kutoka umbali wa futi 4,000 usawa wa bahari, kupitia kamera hii tuliweza kuwachukua kuanzia wakiwa juu hadi wanashuka chini,” alisema Mshana.
Aidha alisema kamera hiyo pia ilitumika wakati wa msiba wa aliyekuwa Rais wa kwanza wa Afrika Kusini Nelson Mandela, kwa televisheni ya SBA kwa ajili ya kuchukulia matukio mbalimbali katika msiba huo.

No comments: