CUF YAWEKA NGUVU MPYA KUSHINDA UCHAGUZI MWAKANI

Mwenyekiti  wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, ambaye juzi usiku aliibuka mshindi na kuendelea kutetea nafasi yake hiyo ndani ya chama, amesema chama kimeweka nguvu mpya ili kuhakikisha kinashinda uchaguzi mkuu nchini ujao.
Profesa Lipumba alisema haya jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Mkutano mkuu na uchaguzi mkuu wa chama hicho unaomalizika leo jijini Dar es Salaam.
Alisema katika mkutano huo, wajumbe wamewataka viongozi hao wapya kuhakikisha wanajipanga ili kushinda kwenye uchaguzi mkuu wa rais , wabunge na madiwani nchini.
" Tumeagizwa na wajumbe na wanachama wa CUF, tuhakikishe tunajipanga ili tushinde na kuongoza uchaguzi ujao", alisema Lipumba.
Alisema kwa kuhakikisha  CUF wanajipanga katika uchaguzi wa wajumbe wa baraza kuu la chama hicho, vijana wengi wamejitokeza kuweka nguvu mpya ili kuhakikisha wanashinda.
Kuhusu Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Lipumba alisema umoja huo utaendelea kuwepo na wanachofanya hivi sasa ni kila chama cha upinzani kujijenga ili kuwa na nguvu ya pamoja .
Akizungumzia kama Ukawa watarejea bungeni kwenye bunge la katiba, Lipumba alisema ikiwa rasimu ya Jaji Warioba ndiyo itajadiliwa, wako tayari kurudi ila kama sio hivyo hawatarejea.
Kwa upande wake mgombea mweza wa nafasi hiyo, Chief Yemba ambaye aliibuka kwa kupata kura 30, kati ya kura 690 alisema ameridhishwa na matokeo ya uchaguzi kwa kuwa yalikuwa huru.
Yemba alisema kura 30 alizopata sio ndogo na kwamba kura za kumfanya ashinde hazikutimia tu na kumpongeza Lipumba kwa ushindi wa kishindo kwa kupata kura 659 kati ya kura 690.Nafasi ya Makamu mwenyekiti ilichukuliwa na Duni haji aliyepata kura 662 na nafasi ya Katibu ilichukuliwa na Maalimu Seif aliyepata kura 675.

No comments: