SUMBAWANGA YAELEMEWA NA WATOTO WA MITAANI



Mji wa Sumbawanga mkoani Rukwa  umetajwa kuwa unaelemewa na  idadi kubwa  ya  watoto  wa mitaani  wanaorandaranda  katika  kona ya  mji  huo, huku  baadhi  yao  wakidaiwa  kutumika  na  makundi ya kihalifu.
Wengi  wa  wadau  wameingiwa  na  hofu kutokana na idadi  kubwa  ya watoto  hao  wenye umri wa  miaka  kati  ya  miaka 3-15, wakidai ni 'bomu'  tarajiwa  iwapo  mamlaka  husika  hazitakuwa na mikakati  dhabiti  ya  kupambana na  tatizo  hilo.
Kwa mujibu  wa Ofisa Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Sumbawanga,  James Biseko, manispaa  hiyo ina idadi ya watoto 7,870 wakiwemo  watoto  wanaishi katika  mazingira magumu  na  wale  wanaoishi mitaani  mjini Sumbawanga.
Hata  hivyo, kutokana  na  idadi  kubwa  ya watoto wanaoishi  mtaani  Mjini Sumbawanga, ofisa huyo amekiri  kuwa  hana  takwimu rasmi  ya watoto  hao.
Uchunguzi  uliofanywa  na mwandishi  wa  habari  hizi  umebaini kuwa  watoto hao  wanaoishi  mitaani  mjini hapa wanaishi  katika  vikundi  wakiwa na uongozi  wao  ambapo  wale wenye umri  mdogo  ndio  'wahasibu'  wa  vikundi hivyo.
Wamekiri  baadhi yao kutumiwa na makundi  ya kihalifu  hususani wale wenye  maumbile madogo  ambapo  wanapitishwa  madirishani  usiku  wakielekezwa  wakiingia ndani  wafungue milango  ya  nyumba kisha 'wahalifu'  hao  huingia  ndani na kuiba .
Kwa upande  wake Kamanda wa Polisi  wa Mkoa  wa Rukwa, Jacob Mwaruanda amekiri  kuwa  watoto  wa mitaani ni tatizo ambalo  linaongezeka  kila kukicha.

No comments: