Watu 247 wametiwa mbaroni kutokana na
makosa mbalimbali baada ya kunaswa katika Operesheni Usalama Namba Moja
iliyofanywa na jeshi la polisi nchini kwa kushirikiana na Polisi wa Kimataifa
(INTERPOL) katika mikoa mbalimbali.
Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi wa
Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Issaya Mngulu wakati akizungumza na
waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam.
Alisema
operesheni tajwa imetokana na maamuzi yaliyofikiwa kwenye mkutano wa
wakuu wa majeshi wa kanda zote mbili na kisha kuwekewa mpango mkakati wa utekelezaji kwenye kikao kilichowakutanisha wakuu wa upelelezi.
Aliongeza kuwa operesheni hii imekuwa
na mafanikio makubwa kwa sababu pamoja na kukamatwa vitu mbalimbali pia
wametuma ujumbe kwa wahalifu kuwa jeshi letu lipo imara kuhakikisha maisha na
mali za watu ziko salama.
Alisema katika operesheni hiyo jumla ya
wahamiaji haramu 84 walikamatwa ambao saba ni kutoka Kongo na 77 kutoka
Burundi, na pia walifanikiwa kukamata madawa ya kulevya heroin gramu 5, bangi
gramu 8, misokoto 195 na mirungi kilo 200.
Pia kwa upande wa wizi wa magari jumla
ya magari 18 yalikamatwa, kati ya magari hayo 11 yaligunduliwa kuingiliwa
chasis na injini namba, magari manne na pikipiki tatu yaligunduliwa kutoka nchi
tofauti kama Afrika Kusini, Japan na Burundi.
Aliongeza kuwa pia walifanikiwa
kukamata silaha haramu pisto moja,
gobori 1 na risasi 3.
Aidha alitoa mwito kwa wananchi kuwa jeshi hilo litaendelea kufanya misako ya
mara kwa mara ili kupunguza uhalifu nchini na pia aliwataka wananchi waendelee
kutoa ushirikiano wao katika harakati za kupambana na uhalifu wa aina yeyote
hapa nchini.
No comments:
Post a Comment