SUMATRA SASA YAKUNJULIA MAKUCHA YAKE UDA



Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) imesisitiza kwamba, mabasi ya Shirika la Usafirishaji Dar es Salaam (UDA) yanatakiwa kupaka rangi kulingana na njia na si kuweka vibao pekee. 
Meneja Mawasiliano wa Sumatra, David Mziray alikiri mamlaka yake, wiki iliyopita, ilitoa agizo kwa Uda kuhakikisha mabasi yake yanapakwa  rangi kama ilivyo kwa daladala za kawaida na kuweka vibao  kuonesha njia wanakotoa huduma. 
Hata hivyo alisema mpaka sasa, shirika hilo halijatekeleza agizo hilo hali ambayo imelazimu mamlaka kukamata mabasi matano  kutokana na kukiuka masharti hayo. 
Mziray alisema kama hawatatekeleza, mamlaka itaendelea kuwakamata.  
“Makubaliano tuliyofanya na Uda ni kupaka rangi na kuweka vibao na si vibao pekee kama Uda wanavyodai,” alisema Mziray. 
Alisisitiza, “Sisi tutaendelea kukamata magari yao kama hawatatekeleza agizo hivyo ni vizuri wakubaliane  ili kuondoa usumbufu.” 
Hayo yamekuja baada ya Uda kutoa taarifa kuwa wamekubaliana na Sumatra kuweka vibao na si rangi kitendo amacho Sumatra wamepinga.
Akizungumza hivi karibuni na mwandishi, Mkuu wa UDA, Hamdy Al Hadj alisema makubaliano yao na Sumatra ni  kuwepo kwa vibao katika magari yao kuonesha njia wanazotoa huduma na si kupaka rangi. 
 “Kwa mfano kama basi linakwenda Gongo la Mboto basi katika kibao kilichoko mbele ya basi kiwe na rangi ya eneo hilo kama ilivyo katika daladala,” alisema Hamdy.
Alisema tayari Shirika hilo linaendelea kukamilisha uwekwaji wa vibao hivyo mbele ya mabasi yote yanayotoa huduma pamoja na kwamba nyuma ya mabasi kumewekwa namba ili abiria waweze kutoa taarifa pindi watakapohudumiwa tofauti.

No comments: